12. Wanawake wa kwanza walikuwa wakijifunika wanapotoka majumbani

3- Imethibiti katika al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali Fajr na wanawake wa waumini wakiswali pamoja naye, wamejigubika mavazi yao. Wanapoenda nyumbani hakuna yeyote awezae kuwajua kwa sababu ya giza.”[1]

Amesema (Radhiya Allaahu ´anhaa) pia:

“Lau Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliona kwa wanawake yale tunayoyaona sisi, basi angeliwakataza kwenda misikitini kama jinsi Banuu Israaiyl walivyowakataza wanawake wao.”

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amepokea mfano wake. Kinacholengwa katika Hadiyth hii ni kifuatacho:

Kwanza: Wanawake wa Maswahabah, ambao walikuwa ni karne bora, walikuwa na ada ya kujisitiri na kujifunika. Wao ni karne tukufu zaidi, bora na kamilifu mbele ya Allaah inapokuja katika tabia, adabu, imani na matendo. Wao ni viigizo. Allaah awawie radhi na wale wenye kuwaiga. Allaah (Ta´ala) amesema:

السَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Na wale waliotangulia awali, miongoni mwa Muhaajiriyn [waliohajiri kutoka Makkah] na Answaar [wakaazi wa al-Madiynah waliowasaida], na wale waliowafuata kwa wema – Allaah Ameridhika nao nao wameridhika Naye: Amewaandalia mabustani ipitayo chini yake mito, humo [watakuwa] ni wenye kudumu milele. Huko ndiko kufuzu kukuu.”[2]

Ikiwa hayo ndio yalikuwa matendo ya Maswahabah, mtu anaweza kujiuliza ni vipi inaweza kutustahikia kwenda kinyume na njia ambayo Allaah (Ta´ala) ameridhika nayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Na yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini; hyuo Tutamgeuza alikogeukia na Tutamuingiza Motoni – na ubaya ulioje marudio ya mwisho!”[3]

Pili: Mama wa waumini ´Aaishah na ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhumaa) – wenye kujulikana kwa elimu, uelewa na umaizi uliyobobea katika dini ya Allaah na kuwatakia mema waja Wake – wameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliwakataza wanawake kwenda misikitini lau angeliona yale wanayoyaona. Hali ilibadilika kiasi kikubwa katika masiku ya karne bora ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mpaka kufikia kuwakataza wanawake kwenda misikitini. Vipi tusemeje leo baada ya miaka elfu moja na mia nne? Mambo yamezidi kuwa mabaya, haya imekuwa ndogo zaidi na dini dhaifu na dhaifu kwenye mioyo ya watu wengi.

Kutokana na ukamilifu wa Shari´ah ´Aaishah na Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wakafahamu kuwa kila kinachopelekea katika uharamu nacho pia haramu.

[1] al-Bukhaariy (372) na Muslim (645).

[2] 09:100

[3] 04:115

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 26/03/2017