12. Uwajibu wa kufuata ´Aqiydah ya Salaf

Uwajibu huo umebainishwa katika Qur-aan, Sunnah na maneno ya maimamu. Ama katika Qur-aan ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, basi tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kurejea!”[1]

Amemtishia Moto yule asiyefuata njia yao. Na amemwahidi yule mwenye kuwafuata radhi na Pepo:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ

“Wale waliotangulia awali miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye.”[2]

50- Katika Sunnah Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu. Tahadharini na mambo yaliyozuliwa, kwani kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila ni upotevu”[3]

Ameamrisha kushikamana barabara na Sunnah za makhaliyfah wake kama alivyoamrisha kushikamana na Sunnah zake. Amebainisha kwamba kila kilichozuliwa ni Bid´ah na upotevu. Hayo ni yale yasiyoafikiana na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Sunnah za  Maswahabah wake.

52- ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ummah wangu utafikwa na yale yaliyowafika wana wa israaiyl hatua kwa hatua. Kiasi cha kwamba kukiwemo katika wao ambaye atamwingilia mama yake hadharani basi atapatikana katika Ummah wangu pia takayefanya hivo. Wana wa israaiyl waligawanyika mapote sabini na mbili  na watagawanyika pote moja zaidi.”[4]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mayahudi waligawanyika mapote sabini na moja. Manaswara waligawanyika mapote sabini na mbili. Na Ummah wangu utakuja kugawanyika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja.” Kukasemwa: “Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile litakalofuata kile ninachofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu”[5]

53- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kwamba kundi lililookoka ni lile litalomfuata yeye na Maswahabah wake. Litakaloenda kinyume nalo linaingia ndani ya yale mapote sabini na mbili ya Motoni. Kwa sababu yule asiyewafuata Salaf (Rahimahumu Allaa) na akaamini kuhusu sifa katika Qur-aan na Sunnah kutoka kichwani mwake mwenyewe kwa njia inayopingana na ´Aqiydah ya Salaf, basi atakuwa amezua na kuleta mambo mepya katika dini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa, kwani kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila ni upotevu.”

[1] 04:115

[2] 09:100

[3] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[4] ash-Shariy´ah, uk. 15

[5] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 13/12/2018