11. Salaf wote walikuwa wakiamini sifa kwa udhahiri wake

39- Abul-Hasan Sa´dullaah bin Naswr bin ad-Dajaajiy ametukhabarisha: Imaam Abu Mansuur Muhammad bin Ahmad al-Khayyaat ametuhadithia: Abu Twaahir ´Abdul-Ghaffaar bin Muhammad bin Ja´far ametuhadithia: Abu ´Aliy bin as-Swawwaaf ametuhadithia: Bishr bin Muusaa ametuhadithia: Abu Bakr ´Abdullaah bin az-Zubayr al-Humaydiy ametuhadithia:

“Katika ´Aqiydah kunaingia vilevile yale yaliyomo katika Qur-aan na Sunnah ikiwa ni pamoja na:

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Bali mikono Yake imefumbuliwa.”[1]

وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ

”Mbingu zitakunjwa mkononi mwake mwa kuume.”[2]

Hatuzidishi juu yake na wala hatufasiri. Tunasimama pale Qur-aan iliposimama na tunasema:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ‘Arshi.”[3]

Mwenye kusema jengine mbali na hili ni Jahmiy mkanushaji.”[4]

40- Yahyaa bin Mahmuud ametukhabarisha: Bababu yagu Haafidhw Abul-Qaasim ametuhadithia:

“Yale yaliyokuja katika Qur-aan na yakapokelewa kwa cheni za wapokezi Swahiyh, basi madhehebu ya Salaf (Rahimahumu Allaah) ni kuyathibitisha, kuyapitisha kwa udhahiri wake na kuyakanushia namna. Kwa sababu kuzugumzia sifa ni kama kuzungumzia dhati. Kuthibitisha dhati ni kuthibitisha uwepo, na si kuthibitisha namna. Vivyo hivyo kuthibitisha sifa. Salaf wote waliamini hivo. Maneno ya Maalik yamekwishatangulia wakati alipoulizwa kuhusu kulingana.”

41- Qurrah bin Khaalid amepokea kutoka kwa al-Hasan,  kutoka kwa mama yake, kutoka kwa Umm Salamah ambaye amesema kuhusiana na:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ‘Arshi.”

“Kulingana si ambako hakufahamiki. Namna haieleweki. Ni wajibu kuamini hilo na ni kukanusha hilo ni kufuru.”[5]

42- Rabiy´ah bin Abiy ´Abdir-Rahmaan amesema:

“Kulingana si ambako hakufahamiki. Namna haieleweki. Ujumbe ni wenye kutoka kwa Allaah, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana jukumu la kufikisha na sisi tuna jukumu la kusadikisha.

43- Maneno haya yamekaribiana maana na matamshi. Inawezekana Maalik na Rabiy´ah walifikiwa na khabari yale yaliyosemwa na Umm Salamah ambapo na wao wakawa wameyaiga kutokana na usahihi wake na uzuri wake na jengine ni kwa sababu alikuwa mmoja katika wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Inawezekana vilevile Allaah (Ta´ala) aliwahidi katika usawa na akawapa ilham ya kuongea maneno ya kisawasawa kama alivyompa ilham Umm Salamah.

44- Maneno yao:

“Kulingana si ambako hakufahamiki.”

Bi maana si ambalo hakufahamiki kuwepo kwake, kwa sababu Allaah ndiye kazungumza hivo. Khabari zake ni za kweli na za yakini ambazo haijuzu kuzitilia shaka. Ikawa si jambo lisilofahamika kulijua. Imepokelewa katika baadhi ya matamshi:

“Kulingana kunajulikana.”

45- Maneno yao:

“Namna haieleweki.”

Hili kwa sababu namna haikutajwa. Hakuna uwezekano wa kulitambua hilo pasi na dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

46- Maneno yao:

“Ni kukanusha hilo ni kufuru.”

Kwa sababu ni kuyarudisha maneno ya Allaah na ni kukufuru maneno ya Allaah. Mwenye kukufuru neno moja ambalo kuna maafikiano juu yake ni kafiri. Tusemeje kwa yule mwenye kukufuru Aayah saba ambazo zimetajwa sehemu mbalimbali saba katika Kitabu cha Allaah (Ta´ala)? Kwa ajili hiyo ndio maana ni wajibu kuamini hilo.

47- Maneno yao:

“Kuuliza hilo ni Bid´ah.”

Kwa sababu ni kuuliza juu ya kitu ambacho hakuna njia ya kukitambua, wala haijuzu kuzungumzia maudhui hayo na wala hilo halikuulizwa katika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala wakati wa Maswahabah.

[1] 05:64

[2] 39:67

[3] 20:05

[4] Usuul-us-Sunnah, uk. 88-91

[5] Ibn Taymiyyah amesema:

”Jibu hili limepokelewa kutoka kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anh), kutoka kwake yeye na kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo cheni ya wapokezi wake si kitu ambacho mtu anaweza kutegemewa.” (Sharh Hadiyth-in-Nuzuul, uk. 34)

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 13/12/2018