Sifa ya nne: Subira kwa aina zake zote:

1 – Kuwa na subira juu ya kumtii Allaah. Ayafanye akiwa ni mwenye kutarajia thawabu zake na akichelea adhabu ya kufanya mapungufu ndani yake.

2 – Kuwa na subira kutomuasi Allaah. Mtu ajiepushe nayo kutokana na ile khatari inayopatikana ndani yake duniani, ndani ya kaburi na Aakhirah. Hazikuangamia nyumati zilizotangulia ambazo Allaah (´Azza wa Jall) ametukhabarisha kwazo ndani ya Qur-aan isipokuwa ilikuwa ni kwa sababu ya maasi. Wako ambao Allaah aliwazamisha, wengine Allaah aliwateremshia umeme, wengine walichukuliwa kwa ukelele angamizi, wengine Allaah akawadidimiza ardhini na wengine wakajeruhiwa[1]. Yote hayo kwa sababu moja ambayo ni kumuasi Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Kwa sababu Allaah anapaswa kutiiwa na si kuasiwa. Kwa hivyo kumuasi Allaah ni jarima na uovu ambao unasababisha ghadhabu, hasira na adhabu Yake yenye kuumiza.

Kwa hiyo miongoni mwa aina za subira ni kusubiri kutomuasi Allaah. Mtu asiyakurubie. Akiyakurubia akimbilie kwa Allaah kutubia hali ya kuwa ni mkweli, mwenye kuomba msamaha na mwenye kunyenyekea mbele ya Allaah. Isitoshe afuatishe ovu kwa jema. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ

“Hakika mema yanaondosha mabaya.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ovu lifuatishie jema litaifuta.”[3]

3 – Kuwa na subira juu ya makadirio ya Allaah, mipango Yake na hukumu Zake juu ya waja Wake. Hakutikisiki kitu chochote, hakuzuki kitu chochote wala jambo lolote lile ulimwenguni isipokuwa Allaah ndiye amekikadiria. Kwa hivyo ni lazima kufanya subira juu ya misiba inayohusiana na nafsi, mtoto, mali na mfano wa hayo miongoni mwa yale ambayo ni mwenendo wa Allaah unaopitika katika ulimwengu huu. Utawaona viumbe yanawapata majanga mbalimbali na mengi. Huyu anapatwa na umasikini, mwengine anapatwa na maradhi, mwengine anapatwa na hamu na dhiki, mwengine anapatwa na khofu na mwengine anapatwa na mambo yaliyomfika. Hakuna yanayomfaa isipokuwa akiwa ni mwenye kusubiri na mwenye kutarajia malipo kutoka kwa Allaah hali ya kuwa ni mwenye kutafuta uso wa Allaah (´Azza wa Jall) na akitaraji thawabu za wenye kufanya subira ambao Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amewabashiria pindi aliposema:

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ

“Wabashirie wenye kusubiri.”[4]

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika si venginevyo wale wenye kusubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.”[5]

Kutokana na ukubwa wa jambo la subira Allaah akamuusia nalo Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kumwambia:

وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ

“Subiri [kumbuka kuwa] haiwi kusubiri kwako isipokuwa kupitia kwa Allaah.”[6]

Akamfunza kwamba subira ni miongoni mwa tabia za Mitume:

فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُلِ

“Basi subiri kama walivyosubiri wenye azimio madhubuti katika Mitume.”[7]

Vilevile Allaah akawasifu wale wenye akili na busara pale aliposema:

إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَلَا يَنقُضُونَ الْمِيثَاقَ وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ

“Hakika si venginevyo wanaozingatia wale wenye akili tu; ambao wanatimiza ahadi ya Allaah na wala hawavunji fungamano na ambao wanaunga yale aliyoamrisha Allaah kuungwa na wanamwogopa Mola wao na wanakhofu hesabu mbaya.”

Mpaka aliposema:

وَالَّذِينَ صَبَرُوا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ

 “Na ambao wamesubiri kwa ajili ya kutafuta uso wa Mola wao na wakasimamisha swalah na wakatoa sehemu ya vileTuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri na wanaepusha ovu kwa zuri – hao watapata mwisho mwema wa makazi ya Aakhirah.”[8]

Ni lazima subira mtu aifungamanishe na kutafuta uso wa Allaah na Pepo. Hatumaanishi ile subira ambayo unataka watu wakusifu kwamba ni mvumilivu. Bali inatakiwa iwe ule uvumilivu ambao mtu anatafuta kwao uso wa Allaah. Kwa sababu ni miongoni mwa aina za ´ibaadah bora na takasifu zaidi ambazo waislamu, waumini na wafanyao Ihsaan wanapaswa kujipamba nayo.

[1] Shaykh (Rahimahu Allaah) anaashiria maneno Yake (Ta´ala):

فَكُلًّا أَخَذْنَا بِذَنبِهِ ۖ فَمِنْهُم مَّنْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِ حَاصِبًا وَمِنْهُم مَّنْ أَخَذَتْهُ الصَّيْحَةُ وَمِنْهُم مَّنْ خَسَفْنَا بِهِ الْأَرْضَ وَمِنْهُم مَّنْ أَغْرَقْنَا ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ

“Basi kila mmoja Tulimchukuwa kumwadhibu kwa mujibu wa dhambi yake; miongoni mwao wale Tuliowapelekea tufani; na miongoni mwao wale waliochukuliwa na ukelele angamizi; na miongoni mwao wale Tuliowadidimiza ardhini; na miongoni mwao Tuliowagharikisha. Na Allaah Hakuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao wenyewe.” (29:40)

[2] 11:114

[3] at-Tirmidhiy (04/312). Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Mishkaah al-Maswaabiyh” (03/1409).

[4] 02:155

[5] 39:10

[6] 16:12

[7] 46:35

[8] 13:19-22

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 23/11/2021