Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.” (al-´Aswr 103 : 01-03)

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametumia dalili juu ya masuala haya manne kwa maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara.”

Ameapa kwa wakati kwamba kila mtu yumo khasarini isipokuwa yule mwenye kusifika kwa sifa hizi nne:

1 – Imani. Kitendo ambacho ni cha ndani ya moyo na masadikisho ya kukata juu ya kila ambacho ni lazima kukiamini kinachohusu dini ya Uislamu kwa ngazi zake zote.

2 – Matendo mema ya viungo vya mwili. Hapa yanakusudiwa yale matendo ya waziwazi kama mfano wa swalah, swawm, zakaah, hajj, jihaad, kutafuta elimu, kuamrisha mema, kukataza maovu, kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) na matendo mengine yanayofanywa na waumini, waislamu na wenye kufanya Ihsaan juu ya uongofu kutoka kwa Allaah kwa viungo vyao vya mwili.

3 – Kuusiana kunako haki. Hazitimii sifa hizi kwa yeyote isipokuwa baada ya kuijua haki. Kwa hivyo jambo linarudi katika elimu. Ikipatikana inakuwa ndio sababu ya kuongozwa kwa mja na uongofu wa wale anaowalingania ili waongoke kwa mwongozo wa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Kuitambua haki kunaingia katika kuusiana kwa haki uingiaji wa kwanza kabisa. Kwa sababu huwezi kuwausia watu haki isipokuwa baada ya kuijua, jambo ambalo ndilo la lazima.

Kuwausia watu haki kuna ngazi mbalimbali za kutofautiana kwa kutegemea na kutofautiana kwao katika kuijua haki. Huyu anausia haki kwa njia ya ujumla na mwengine anausia haki kwa njia ya upambanuzi. Allaah amesema:

فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا

”Mabonde yakatiririka [maji] kwa kadiri yake.”[1]

Kila mmoja kutegemea na hali yake na uwezo wake.

Katika kilele cha haki ambacho ni lazima watu kuusiana ni kumpwekesha Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Kumpwekesha katika matendo Yake, ´ibaadah Zake na majina na sifa Zake. Kisha kunafuatia faradhi ambazo Allaah (´Azza wa Jall) amewafaradhishia waja Wake kwa aina zake mbalimbali. Muhimu zaidi ni swalah baada ya shahaadah mbili. Kisha mwenzake ni zakaah. Halafu nguzo zengine za Uislamu, imani na Ihsaan.

[1] 13:17

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 23/11/2021