03. Msimamo kwa mume mwenye tabia njema lakini haswali msikitini

Swali 03: Mume wangu ni mwenye tabia njema lakini haswali msikitini na wala haswali swalah zilizopendekezwa. Ninapojaribu kumwamsha Fajr ananifokea usoni jambo ambalo limepelekea kutojaribu kumwamsha ili asinifokee usoni. Wakati mwingine anatoa sababu kwamba hafanyi kitu kinachomkasirisha Allaah, kwamba ni mwenye moyo msafi na anasema kuwa hivo inatosha. Tunaomba mwongozo na nasaha[1].

Jibu: Ni wajibu kwa kila muislamu ambaye ´ibaadah ni zenye kumuwajibikia kuswali swalah tano pamoja na waislamu msikitini. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah na rukuuni pamoja na wanaorukuu.”[2]

وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ

“Utapokuwa upo kati yao ukawaswalisha, basi lisimame kundi miongoni mwao pamoja nawe na wabebe silaha zao.”[3]

Ikiwa ni lazima kuswali kwa mkusanyiko katika hali ya khofu basi uwajibu wake katika hali ya amani kutakuwa na haki zaidi.

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayesikia wito na asiutikie basi hana swalah isipokuwa kutokana na udhuru.”[4]

Ameipokea Ibn Maajah, ad-Daaraqutwniy, Ibn Hibbaan na al-Haakim kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliulizwa: “Ni upi udhuru?” Akasema: “Khofu au maradhi.”

Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba:

“Bwana mmoja kipofu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[5]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Anayetaka kukutana na Allaah kesho hali ya kuwa muislamu basi azihifadhi swalah hizi pindi zinaponadiwa. Hakika Allaah amemuwekea Nabii Wenu njia za uongofu – nazo ni njia za uongofu. Endapo mtaswali majumbani mwenu kama anavoswali nyumbani kwake huyu anayebaki nyuma basi mtakuwa mmeiacha njia ya Mtume wenu. Mkiacha njia ya Mtume wenu basi mtapotea. Tulikuwa tukiona hakuna anayeiacha [swalah ya mkusanyiko] isipokuwa ni mnafiki ambaye unatambulika unafiki wake au mgonjwa. Mtu alikuwa akibebwa kati ya watu wawili mpaka anasimamishwa katika safu.”[6]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Kwa hiyo ni lazima kwako kumnasihi kwa usulubu mzuri na kumpendezea kuswali swalah zilizopendekezwa sambamba na faradhi. Nazo ni Rak´ah nne kabla ya Dhuhr ambapo anatoa Tasliym kila baada ya Rak´ah mbili, Rak´ah mbili baada ya Dhuhr, Rak´ah mbili baada ya Maghrib, Rak´ah mbili baada ya ´Ishaa na Rak´ah mbili kabla ya swalah ya Subh. Jumla zote ni Rak´ah kumi na mbili ambazo huitwa “Rawaatib”. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akizihifadhi na akisema:

“Yeyote anayeswali katika mchana na usiku wake Rak´ah kumi za kujitolea, basi atajengewa kwazo nyumba Peponi.”[7]

Imesihi kutoka kwa Umm Habiybah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba alifasiri Rak´ah hizi kwa Rawaatib zilizotajwa.

Pia imependekezwa kwa muislamu kuswali kabla ya ´Aswr Rak´ah nne. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amrehemu mtu anayeswali kabla ya ´Aswr Rak´ah nne.”[8]

Bora ni yeye atoe Tasliym kila baada ya Rak´ah mbili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku na mchana ni [Rak´ah] mbilimbili.”[9]

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Bora vilevile ni yeye aswali baada ya Dhuhr Rak´ah nne kama alivyoswali kabla yake Rak´ah nne na alete Tasliym kila baada ya Rak´ah nne. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuhifadhi [Rak´ah] nne kabla ya Dhuhr na [Rak´ah] nne baada yake, basi Allaah atamuharamishia Moto.”[10]

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Umm Habiybah (Radhiya Allaahu ´anhaa), mkewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ni lazima kwa mumeo kutahadhari kuchelewesha swalah ya Fajr nje ya wakati wake. Hiyo ni kufuru kubwa kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swalah.”[11]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

 Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tena:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yule atakayeiacha amekufuru.”[12]

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Buraydah bin al-Huswayb (Radhiya Allaahu ´anh).

Hadiyth kuhusu ukubwa wa shani ya swalah na mahimizo ya kuitekeleza ndani ya wakati wake na katika mkusanyiko ni nyingi sana. Namwomba Allaah amwongoze mumeo na waislamu wengine wote katika kila kheri, amlinde dhidi ya shari ya nafsi na matamanio yake na akujaalie kuwa miongoni mwa wasaidizi wake bora katika kheri. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kusikia, yukaribu.

Kuhusu maneno ya mumeo kwamba hafanyi kitu kinachomkasirisha Allaah na kwamba ni mwenye moyo msafi, huko ni kujighuri na ni kuitakasa nafsi. Hapana shaka kwamba kuichelewesha swalah nje ya wakati wake na kutoiswali mkusanyiko msikitini yote mawili ni yenye kumkasirisha Allaah (Subhaanah). Hapana shaka kwamba moyo msafi ambao Allaah ameujaza imani na uchaji Allaah haucheleweshi swalah nje ya wakati wake na wala habaki nyuma kuswali katika mkusanyiko msikitini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Zindukeni! Hakika ndani ya mwili kuna kipande cha nyama. Kinapotengemaa, basi mwili mzima hutengemaa, na kinapoharibika, basi mwili mzima huharibika. Zindukeni, nacho ni moyo.”[13]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/14-21)

[2] 02:43

[3] 04:102

[4] Ibn Maajah (785).

[5] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

[6] Muslim (1046).

[7] Ahmad (26228) na Muslim (728).

[8] at-Tirmidhiy (430) na Abu Daawuud (1271).

[9] at-Tirmidhiy (597) na Ibn Maajah (1322).

[10] Ahmad (26232), at-Tirmidhiy (428) na Abu Daawuud (1269).

[11] Muslim (82).

[12] Ahmad (21859) na at-Tirmidhiy (2545).

[13] Ahmad (27638), al-Bukhaariy (52) na Muslim (1599).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 22-27
  • Imechapishwa: 23/11/2021