12. Ni ipi hukumu ya ambaye alikuwa mgonjwa na akaingiliwa na Ramadhaan?

Swali 12: Ni ipi hukumu ya ambaye alikuwa mgonjwa na akaingiliwa na Ramadhaan na asiweze kufunga kisha akafa baada ya Ramadhaan – je, mtu huyu alipiwe au alishiziwe?

Jibu: Muislamu akifa katika maradhi yake baada ya Ramadhaan, basi halipiwi wala halishiziwi. Kwa sababu alikuwa na udhuru wa Kishari´ah. Hali kadhalika msafiri akifa safarini mwake au punde tu baada ya kufika kutoka safarini mwake si lazima kumlipia wala kumlishizia. Kwa sababu pia huyu alikuwa na udhuru wa Kishari´ah.

Ama kuhusu yule ambaye atapona kutoka katika maradhi yake na akapuuza kulipa mpaka akafa au mtu ametoka safarini mwake na akapuuza kulipa mpaka akafa, basi ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa wale mawalii wao ambao ni wale nduguzo kuwalipia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufa ilihali juu yake kuna swawm, basi amlipie nduguye.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Isipokuwa wepesi kupatikana watakaowafungia, basi wawatolee chakula kumpa masikini kwa kila siku moja waloacha, ambayo ni nusu pishi. Kiwango chake ni 1,5 kg kama anavotakiwa kufanya mzee mtumzima asiyeweza kufunga na mgonjwa ambaye maradhi yake hayatarajiwi kupona, kama ilivyokwishatangulia katika jibu la swali la tisa. Vivyo hivyo mwanamke mwenye hedhi na mwanamke mwenye damu ya uzazi wakipuuza kulipa mpaka wakafa, basi wanatakiwa kutolewa chakula kumpa masikini kwa kila siku moja waloacha. Hapa ni pale ambapo itakuwa si rahisi kuwapata watu wa kuwalipia. Yule ambaye hakuacha mirathi ambayo kutaweza kutolewa chakula hicho basi hakuna kinachomlazimu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[2]

[1] 02:286

[2] 64:16

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdllaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah tata´alaqah bisw-Swiyaam, uk. 20-21
  • Imechapishwa: 21/04/2019