12. Matendo yetu tayari yamekwishakadiriwa

Qadar ni yale yote ambayo Allaah amewakadiria waja Wake katika kheri na shari, imani na kufuru, furaha na kutokuwa na furaha, utajiri na ufukara, maradhi na afya na mengineyo. Hayo yanathibitishwa na Hadiyth Swahiyh ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika!” Kuanzia hapo ikaandika yote yatayokuwepo mpaka kisimame Qiyaamah.”[1]

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Allaah amepanga makadirio ya kila kitu miaka elfukhamsini kabla ya kuumba mbingu na ardhi na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”[2]

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Yale tunayofanya tayari yamekwishapangwa au bado hayajapangwa?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni mambo tayari yamekwishapangwa.” Maswahabah wakasema: “Basi si tuache kufanya matendo na tutegemee yale tuliyokadiriwa?” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Fanyeni matendo! Kwani hakika kila mmoja ni mwenye kufanyiwa wepesi kwa lile aliloumbiwa.”[3]

Kwa hiyo ni wajibu kuamini Qadar na kujisalimisha nayo. Yule asiyeamini Qadar basi hana fungu lolote katika Uislamu. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Yahyaa bin Ya´mar ambaye amesema:

“Mtu wa kwanza kupinga Qadar huko Baswrah alikuwa ni Ma´bad al-Juhaniy. Mimi na Humayd bin ´Abdir-Rahmaan al-Humayriy tukaondoka hali ya kuwa ni wenye kuhiji, au kufanya ´Umrah, tukitaraji kukutana na mmoja katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili tumuulize juu ya yale yanayosemwa na watu hawa kuhusu Qadar. Tukajaaliwa kumuona ´Abdullaah bin al-Khattwaab akiwa ndani ya msikiti. Tukamsogelea, mmoja wetu akiwa upande wake wa kulia na mwingine akiwa upande wake wa kushoto. Nikamdhania rafiki yangu kwamba anataka mimi ndiye nizungumze ambapo nikasema: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Kumejitokeza kati yetu kundi la watu wanaosoma Qur-aan na wanajifunza elimu, hawaamini Qadar na wanaona kwamba hakuna chochote kilichopangwa.” Akasema: “Ukikutana na watu hao, basi waeleze kwamba mimi niko mbali kabisa nao na kwamba wao wako mbali kabisa nami. Ninaapa kwa Yule ambaye ´Abdullaah bin ´Umar anaapa Kwake! Lau mmoja wao angelitoa dhahabu mfano wa mlima wa Uhud, basi Allaah asingeikubali kutoka kwake mpaka aamini Qadar.”[4]

Kinachokusudiwa ni kwamba ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amejitenga mbali na wale wanaopinga Qadar. Hadiyth hizi zimethibiti na ni wajibu kwetu kuziamini na kuamini yale zilizobebea hali ya kuwa ni wenye yakini na wenye kutaka kabisa pasi na mashaka yoyote.

[1] Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (2017).

[2] Muslim (2653).

[3] al-Bukhaariy (4949) na Muslim (2647).

[4] Muslim (8).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 89-91
  • Imechapishwa: 04/04/2019