Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa Sunnah za lazima ambazo mwenye kuacha kipengele chake na akaacha kuikubali na kuiamini hawi katika watu wake. Miongoni mwa Sunnah hizo ni kuamini Qadar, kheri na shari yake na kusadikisha Hadiyth juu yake. Maswali kama “Kwa nini?” na “Vipi?” hayatakiwi kuulizwa. Kinachotakiwa ni kusadikisha na kuamini tu. Yule menye kufikiwa na Hadiyth ambayo haielewi basi atambue kuwa kuna wenye kuielewa na kuimairi kwa ajili yake. Linalompasa ni kuiamini na kuisadikisha. Haijuzu kuwamakinisha akili zao zinazoikadhibisha Hadiyth pamoja na kwamba ni Swahiyh. Haifai kwa muislamu kukadhibisha kitu kama hichi.

MAELEZO

Maneno yake “Miongoni mwa Sunnah” bi maana njia na mfumo. Sunnah imegawanyika mafungu mawili na kunakusudiwa mambo mawili:

1- Njia na mfumo aliokuwa akipita juu yake Mtuem wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Katika kifungu hichi kunaingia ndani yake mambo ya wajibu na yaliyopendekezwa. Kunasemwa miongoni mwa Sunnah ni kitendo fulani. Jambo hilo linaweza kuwa la wajibu, kama mfano wa kuacha ndevu na kuvaa nguo ilio juu ya kongo mbili za miguu, na inawezekana vilevile ikawa ni jambo lililopendekezwa, kama kupeana na kupokea kitu kwa mkono wa kulia.

2- Hukumu ilio chini ya wajibu na inahusiana na matendo bora na mengineyo. Istilahi hii inatumiwa na Fuqahaa´. Kwa mfano wa Hadiyth:

“Mtume alikuwa akipenda kutumia upande wa kulia wakati wa kuvaa kwake viatu, kujichanua kwake, kujisafisha kwake na katika mambo yake mengine yote.”[1]

Bi maana ni mambo yaliyopendekezwa. Imependekezwa kuanza kwa upande wa kulia. Inapokuja katika mambo ya wajibu basi yanaingia katika lile fungu la kwanza. Mfano wa matendo hayo ni kama kula kwa mkono wa kulia, kuachia ndevu na kufupisha masharubu.

[1] al-Bukhaariy (5854) na Muslim (268).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 88-89
  • Imechapishwa: 04/04/2019