10. Fadhilah za kuifuata Sunnah

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Katika Sunnah hakuna kipimo [Qiyaas]. Sunnah hailinganishwi na kitu kingine. Haifahamiki kwa akili wala matamanio. Inahusiana tu na kufuata na kuacha matamanio.”

MAELEZO

Kinachomaanishwa ni kwamba haifai kutumia kipimo katika ´Aqiydah na maandiko ya ´Aqiydah. Kipimo kinatumiwa katika hukumu za mataga. Wakati Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) alipoeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kutawadha tena kwa kula kila kitu kilichopikwa, mmoja katika Maswahabah akasema: “Ni kwa nini hukuwaamrisha kutawadha tena kwa sababu ya maji ya moto?” Ndipo Abu Hurayrah akasema:

“Ee mtoto wa ndugu yangu! Ninapokueleza Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi usiilinganishe na kitu kingine.”[1]

Kusema kwamba hakuna kipimo katika Sunnah kama tulivosema kunamaanishwa katika mambo ya ´Aqiydah.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkemea Haml bin an-Naabighah wakati aliposema:

“Ee Mtume wa Allaah! Ni vipi nitamtolea kafara ambaye hakunywa wala kula, hakuzungumza wala kupiga ukelele? Je, mtu kama huyo anatolewa kafara?” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Unashairi kama wanavyoshairi makuhani?”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Hakika huyu si vyengine isipokuwa ni katika ndugu wa makuhani kwa sababu ya maneno ya vina aliyonena.”[2]

Kujengea juu ya hili haifai kuilinganisha Sunnah na kitu kingine kwa sababu ya kutaka kuiepuka na kutoitendea kazi. Pindi mja anaposikia Hadiyth Swahiyh basi anapaswa kuiamini na wala asitumie kipimo au akakinzana nayo kwa sababu ya maoni ya watu wengine kwa sababu tu ya kutaka kukwepa Sunnah hiyo. Bali ni wajibu kuiamini japokuwa itaenda kinyume na akili za mtu. Mfano wa hayo ni ile Hadiyth iliopokelewa na al-Bukhaariy kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika wa mauti alikuja kwa Muusa bin ´Imraan (´alayhis-Salaam) na akamwambia: “Muitikie Mola wako! Muusa (´alayhis-Salaam) akalipiga jicho la Malaika wa mauti mpaka likaanguka. Malaika wa mauti akarudi kwa Allaah (Ta´ala) akamwambia: “Umenituma kwa mmoja katika waja Wako asiyetaka kufa. Amenipiga jicho langu.” Allaah akamrudishia jicho lake na akasema: “Rudi kwa mja Wangu na umwambie: “Wewe unachotaka ni kuishi? Ikiwa unachotaka ni kuishi basi weka mkono wako juu ya mgongo wa ng´ombe. Utaishi miaka kwa kiasi cha kila unywele mmoja utaogusa mkono wako.” Akasema: “Kisha baadaye itakuweje?” Akamjibu: “Kisha baadaye utakufa.” Akasema: “Basi nachagua kufa hivi sasa.” Mola wangu! Nakuomba nifikishe katika ardhi Tukufu mahali pa kurusha mawe!” Naapa kwa Allaah! Lau ningekuwepo huko basi ningekuonyesheni kaburi lake karibu na njia pembezoni na pedi udongo mwekundu.”[3]

Huenda baadhi ya watu wakaielewa Hadiyth kama jambo ambalo haliwezi kutokea kwa sababu akili zao hazilisadikishi. Matokeo yake wakaikadhibisha pamoja na kwamba Hadiyth ni Swahiyh na imepokelewa na al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake. Haijuzu kwa muislamu kuikadhibisha.

[1] at-Tirmidhiy (79) na Ibn Maajah (22). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah”.

[2] al-Bukhaariy (5758) na Muslim (1681).

[3] al-Bukhaariy (1339) na Muslim (2372).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 85-87
  • Imechapishwa: 04/04/2019