12. Hakuna mbora wa maneno kama mlinganizi

Miongoni mwa yaliyomo ndani katika Aayah hii tukufu:

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

“Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania watu kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu?”[1]

Maana yake ni kwamba hakuna yeyote ambaye ana maneno mazuri zaidi kumshinda yeye kwa sababu amelingania kwa Allaah, akaelekeza Kwake na akatendea kazi yale anayolingania. Kwa msemo mwingine ni kwamba amelingia katika haki na akaitendea kazi na sambamba na hilo akakemea batili, akaitahadharisha na kuiacha. Ukiongezea juu ya kwamba akasema wazi yale aliyomo na hakuona hayaa. Bali amesema wazi kwamba yeye ni miongoni mwa waislamu. Anafurahishwa kwa yale ambayo Allaah amemneemesha. Hawi kama ambaye anaona bezo kutokana na jambo hilo na akachukia kusema kuwa ni muislamu au ya kwamba analingania katika Uislamu kwa sababu ya kumzingatia fulani au kumpaka mafuta fulani. Hapana matikiso wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Bali muumini anayelingania kwa Allaah, mwenye imani yenye nguvu na mtambuzi wa amri ya Allaah anasema kwa marefu na mapana kuhusu haki ya Allaah, anapata uchangamfu katika kulingania katika dini Yake na anatendea kazi yale anayolingania kwayo. Sambamba na hilo ajiepushe na yale anayokataza. Kwa msemo mwingine ni kwamba awe miongoni mwa watu wepesi zaidi katika yale anayolingania na miongoni mwa watu waliojitenga zaidi na yale anayokataza. Pamoja na yote haya aseme waziwazi kuwa yeye ni muislamu na kwamba analingania katika Uislamu. Aidha afurahi kwa jambo hilo. Amesema (´Azza wa Jall):

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ

“Sema: “Kwa fadhilah za Allaah na kwa rehema Zake, basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.”[2]

Kufurahi kwa rehema na fadhilah za Allaahni furaha inayokubalika katika Shari´ah. Lakini furaha iliyokatazwa ni ile furaha ya kiburi. Hiyo ndio furaha iliyokatazwa. Amesema (´Azza wa Jall) kuhusu kisa cha Qaaruun:

لَا تَفْرَحْ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْفَرِحِينَ

”Usifurahi kwa jeuri; hakika Allaah hawapendi wanaofurahi kwa jeuri.”[3]

Hii ni furaha ya kiburi, furaha ya kujiweka juu ya watu na kujikweza. Hii ndio furaha iliyokatazwa. Kuhusu kufurahi kwa ajili ya dini ya Allaah, kufurahia uongofu wa Allaah, kujipa bishara njema kwa jambo hilo na kusema hilo kwa kinywa kipana ni jambo limewekwa katika Shari´ah na lenye kusifiwa.

Aayah hii tukufu ni miongoni mwa Aayah zilizo wazi kabisa zinazofahamisha juu ya ubora wa ulinganizi, kwamba ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi ya kujikurubisha kwa Allaah, kwamba ni miongoni mwa matendo bora kabisa na kwamba watu wake wako katika upeo wa hali ya juu kabisa wa utukufu na katika vyeo vya juu kabisa. Wanaoshika nafasi za juu kabisa ni Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Wakamilifu zaidi katika jambo hilo ni yule wa mwisho wao na kiongozi wao Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhiwa sallam).

[1] 41:33

[2] 10:58

[3] 28:76

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 04/06/2023