Zipo Aayah na Hadiyth nyingi zilizopokelewa kuhusu ubora wa ulinganizi na walinganizi. Ni kama ambavo kumepokelewa Hadiyth nyingi zinazotambulika kwa wanazuoni juu ya kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwatuma walinganizi. Miongoni mwazo ni maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

“Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania watu kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu?”[1]

Aayah hii tukufu inawasifia walinganizi na kwamba hakuna yeyote ambaye ana maneno mazuri kuwashinda wao. Katika kilele chao wako Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kisha wafuasi wao kutegemea daraja zao katika kulingania, elimu na ubora. Wewe, ee mja wa Allaah, inakutosha kuwa utukufu kwa kuwa ni miongoni mwa wafuasi wa Mitume.

[1] 41:33

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 20-21
  • Imechapishwa: 04/06/2023