12. ´Aqiydah sahihi juu ya Maswahabah

Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwapenda Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kujenga urafiki nao, kuwatakia radhi na kuwaombea msamaha na kuwasifia. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Na wale waliotangulia wa mwanzo miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema – Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” (09:100)

Allaah (Ta´ala) amewaridhia waliotangulia mwanzoni pasi na kushurutisha wema. Kuhusu wale waliokuja nyuma, hayuko radhi na wao endapo hawatowafuata kwa wema. Amesema (Ta´ala):

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ

“Kwa hakika Allaah amewawia radhi waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu chini ya mti.” (48:18)

Yule ambaye Allaah ameridhika naye basi hatomkasirikia maishani. Imethibiti katika Hadiyth Swahiyh ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna yeyote aliyetoa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti atayeingia Motoni.”

Allaah amewaelezea Muhaajiruun na kuwasifu ya kwamba ni wakweli. Amesema (Ta´ala):

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Kwa ajili ya mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na [zikataifishwa] mali zao wanatafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake. Hao ndio wakweli.” (59:08)

Halafu Akawataja Answaar na kusema:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Na wale waliokuwa na makazi na wakawa na imani kabla yao wanawapenda wale waliohajiri kwao na wala hawapati kuhisi choyo yoyote vifuani mwao kwa yale waliyopewa, na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe ni wahitaji. Na yeyote anayeepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.” (59:09)

Kisha Akataja (Ta´ala) hali za waumini baada yao wenye kuwafuata Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa wema na kusema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.” (59:10)

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huo ni mfano wao katika Tawraat na mfano wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake liwapendezeshe wakulima ili kuwakasirisha makafiri. Allaah amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema miongoni mwao msamaha na ujira mkubwa.” (48:29)

Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule ambaye moyoni mwake mna chuki dhidi ya mmoja katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi anaingia ndani ya Aayah hii. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ

“Na wale walioamini na wakahajiri na wakafanya jihaad katika njia ya Allaah na wale waliotoa makazi na wakanusuru – hao ndio waumini wa kweli. Watapata msamaha na riziki tukufu.” (08:74)

Amesema (Ta´ala) juu ya Maswahabah akibainisha fadhilah za wale waliojitolea na kupigana kabla ya Ushindi – mkataba wa Hudaybiyah – juu ya wale waliojitolea na kupigana baada ya Ushindi – lakini makundi yote mawili yameahidiwa Pepo na Allaah:

لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ أَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

“Hawi sawa miongoni mwenu aliyetoa kabla ya Ushindi na akapigana. Hao watapata daraja za juu kabisa kuliko wale waliotoa baada [ya ushindi] na wakapigana – na wote Allaah amewaahidi Pepo. Na Allaah kwa yote myatendayo ni Mjuzi.” (57:10)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwatukane Maswahabah zangu.”

Katika matamshi ya Muslim imekuja:

“Msimtukane yeyote katika Maswahabah zangu. Lau atakuwepo mtu atayetoa dhahabu mfano wa [mlima wa] Uhud, basi hautofikia viganja viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu bora ni karne yangu, kisha wataofuatia, kisha wataofuatia.” ´Imraan amesema: “Sijui alisema karne mbili au tatu baada ya karne yake.” Halafu baada ya hapo watakuja watu wataotoa ushuhuda pasi na kuombwa kushuhudia, watafanya khiyana pasi na kuaminiwa, wataweka nadhiri pasi na kutimiza na kutadhahiri kwao kuipenda dunia.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya Answaar:

“Alama ya imani ni kuwapenda Answaar. Alama ya unafiki ni kuwachukia Answaar.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Answaar:

“Hakuna anayewapenda isipokuwa muumini tu na hakuna anayewachukia isipokuwa mnafiki tu. Allaah anampenda yule mwenye kuwapenda na Allaah anamchukia yule mwenye kuwachukia.”

Muslim amepokea kutoka kwa Abu Hurayrah na Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mtu anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho anayewachukia Answaar.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu kisa cha Haatwib bin Abiy Balt´ah:

“Ameshuhudia [vita vya] Badr. Allaah aliwatazama watu wa Badr na kusema: “Fanyeni mtakalo, hakika Nimekusameheni.”

Muslim amepokea kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema kuwa Umm Mubashshir alimsimulia ya kwamba alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema kwa Hafswah:

“Hakuna yeyote katika wale waliokula kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti atayeingia Motoni – Allaah akitaka.”

Walikuwa watu zaidi ya 1400 na miongoni mwao alikuwa Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy.

Ahl-us-Sunnah wanaitakidi kuwa mbora wa Ummah huu baada ya Manabii wake ni Abu Bakr as-Swiddiyq. Kisha ´Umar al-Faaruq. Haya ni kwa maafikiano ya Maswahabah na Taabi´uun. Hakuna yeyote katika wao aliyepingana na hili.

Kumepokelewa mapokezi tele kutoka kwa kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema:

“Wabora wa Ummah huu baada ya Manabii wake ni Abu Bakr na ´Umar.”

Ahl-us-Sunnah wanaonelea kuwa watatu ni ´Uthmaan na wanne ni ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 77-82
  • Imechapishwa: 21/06/2020