13. ´Aqiydah sahihi juu ya watu wa nyumbani kwa Mtume

Katika ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni pamoja na kuwapenda watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutambua fadhilah na utukufu wao. Katika hali hii mtu anatakiwa kutendea kazi wasia wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Ghadiyr Khumm. Alimhimidi Allaah na akamsifu, akawaidhisha na kukumbusha. Kisha akasema:

“Amma ba´d: Enyi watu! Hakika mimi si mwingine isipokuwa ni mwanadamu tu. Anakaribia mjumbe kutoka kwa Mola wangu kunijia [kunichukua] na hapo itabidi niitikie. Nimekuachieni vitu viwili. Cha kwanza ni Kitabu cha Allaah ambacho ndani yake mna uongofu na nuru. Hivyo basi kichukueni Kitabu cha Allaah na shikamaneni nacho.”

Akasisitiza juu ya Kitabu cha Allaah halafu akasema:

“Na familia yangu. Ninakukumbusheni Allaah juu ya familia yangu. Ninakukumbusheni Allaah juu ya familia yangu. Ninakukumbusheni Allaah juu ya familia yangu.”

Ibn Kathiyr amesema katika Tafsiyr yake:

“Hatuukatai wasia wa watu wa nyumbani kwa Mtume na kuwatendea wema, kuwaheshimu na kuwatukuza. Hakika wanatokamana na kizazi kisafi na familia tukufu kabisa iliyopo katika uso wa ardhi kifakhari, kiukoo na kinasabu. Hili khaswa pale ambapo watakuwa ni wenye kufuata Sunnah ya kinabii, sahihi na ilio wazi. Hali kama hii ndio waliokuwa nayo wahenga wao kama al-´Abbaas na watoto wake na ´Aliy na familia yake na dhuriya yake – Allaah awawie radhi wote.”

Miongoni mwa watu wa familia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wakeze. Amesema (Ta´ala) kuhusu wao:

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ لَطِيفًا خَبِيرًا

“Na bakieni majumbani mwenu na wala msionyeshe mapambo uonyeshaji mapambo wa zama za ujahili na simamisheni swalah na toeni zakaah na mtiini Allaah na Mtume Wake. Hakika si vyenginevyo Allaah anataka akuondosheeni uchafu, enyi watu wa nyumba na akutakaseni mtakaso barabara. Na yakumbukeni yale yanayosomwa majumbani mwenu katika Aayah za Allaah na hekima, hakika Allaah daima ni Mjuzi, Mwenye khabari ya yote.” (33:33-34)

Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema katika Tafsiyr yake:

“Aayah hii ni dalili ya wazi juu ya kwamba wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanaingia katika familia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu wao ndio sababu ya kuteremka kwa Aayah. Sababu ya kuteremka kwa Aayah na kwamba inaingia ndani yake ni jambo lisilokuwa na tofauti juu yake. Ima inaingia na kutumika hiyo tu, jambo ambalo ni moja katika maoni, au hiyo na nyenginezo, jambo ambalo ndio maoni sahihi zaidi.”

Katika Aayah hii ameingia kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib, Faatwimah msichana wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhum). Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka asubuhi akiwa na kitambara kilicho na michoro wa mkoba wa ngamia wenye manyoa meusi ambapo akaja al-Hasan bin ´Aliy akamwingiza ndani yake, akaja al-Husayn akaingia pamoja naye kisha akaja Faatwimah akamwingiza. Halafu akasema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا

“Hakika si vyenginevyo Allaah anataka akuondosheeni uchafu, enyi watu wa nyumba na akutakaseni mtakaso barabara.” (33:33-34)

Ameipokea Muslim.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 83-85
  • Imechapishwa: 21/06/2020