Abu Bakr bin Zakariyyaa ash-Shaybaaniy ametukhabarisha: Nimemsikia Abu Haamid ash-Sharqiy: Nimemsikia Hamdaan as-Sulamiy na Abu Daawuud al-Khaffaaf: Tumemsikia Ishaaq bin Ibraahiym al-Handhwaliy akisema:

”Gavana ´Abdullaah bin Twaahir alinambia: ”Ee Abu Ya´quub! Hadiyth hii unayosimulia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ”Anashuka Mola wetu (´Azza wa Jall) kila usiku katika mbingu ya chini” – anashuka vipi?” Nikasema: ”Allaah akutie nguvu ee gavana! Hakuulizwi juu ya Mola (´Azza wa Jall) vipi. Hakika mambo yalivyo ni kwamba anashuka bila namna.”

Abu Ya´quub Ishaaq bin Ibraahiym al-´Adl ametuhadithia: Mahbuub bin ´Abdir-Rahmaan al-Qaadhwiy ametuhadithia: Babu yangu Abu Bakr Muhammad bin Ahmad bin Mahbuub amenihadithia: Ahmad bin Hamuuyah ametuhadithia: Abu ´Abdir-Rahmaan al-´Atakiy ametuhadithia: Muhammad bin Salaam ametuhadithia:

”Nilimuuliza ´Abdullaah bin Mubaarak juu ya kushuka usiku wa nusu Sha´baan. Akajibu: ”Ee mnyonge, Anashuka kila usiku.” Bwana mmoja akasema: ”Ee Abu ´Abdillaah! Anashuka vipi? Je, huacha maeneo hayo?” ´Abdullaah akasema: ”Anashuka anavyotaka.”

Imekuja katika upokezi mwingine ´Abdullaah bin al-Mubaarak alimwambia bwana huyo:

”Unapofikiwa na Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi jisalimishe nayo.”

Nimemsikia Haafidhw Abu ´Abdillaah al-Haakim: Nimemsikia Abu Zakariyyaa Yahyaa bin Muhammad al-´Anbariy: Nimemsikia Ibraahiym bin Abiy Twaalib: Nimemsikia Ahmad bin Sa´iyd bin Ibraahiym Abu ´Abdillaah ar-Ribaatiy akisema:

”Siku moja nilihudhuria kwa gavana ´Abdullaah bin Twaahir. Ishaaq bin Ibraahiym – yaani Ibn Raahuuyah – naye akahudhuria. Akaulizwa kuhusu Kushuka na kama ni Swahiyh. Akajibu: ”Ndio.” Ndipo mmoja katika makamanda wa ´Abdullaah akasema: ”Ee Abu Ya´quub, unadai kuwa Allaah (Ta´ala) anashuka kila usiku?” Akajibu: ”Ndio.” Akasema: ”Anashuka vipi?” Ndipo Ishaaq akamwambia: ”Nithibitishie ujuu Wake, ili nikueleze Ushukaji.” Bwana yule akasema: ”Nathibitisha kuwa Kwake juu.” Ishaaq akasema: ”Allaah (´Azza wa Jall) amesema.

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا

“… na atakapokuja Mola wako na Malaika safu kwa safu.”[1]

Gavana ´Abdullaah akasema: ”Ee Abu Ya´quub! Hilo litatokea siku ya Qiyaamah.” Ndipo Ishaaq akasema: ”Allaah akutie nguvu ee gavana! Ni nani awezaye kumzuia kuja leo Yule ambaye Atakuja siku ya Qiyaamah?”

[1] 89:22

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 193-198
  • Imechapishwa: 05/12/2023