11. Ahl-ul-Hadiyth wanathibitisha kushuka na kuja kwa Mola

Ahl-ul-Hadiyth wanathibitisha kushuka kwa Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) kila usiku katika mbingu ya chini, bila ya kumfananisha na kushuka kwa viumbe, wala kumlinganisha wala kumfanyia namna. Bali wanamthibitishia yale aliyomthibitishia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hawasemi kitu zaidi yake. Wanayapitisha maelezo sahihi yaliyopokelewa juu yake kwa udhahiri wake na wanamtegemezea ujuzi wake Allaah.

Aidha wanamthibitishia mengine yote aliyoyataremsha Allaah ndani ya Kitabu Chake, kukiwemo kuja na ujio Wake, yaliyotajwa katika maneno Yake (´Azza wa Jall):

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

“Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”[1]

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا

“… na atakapokuja Mola wako na Malaika safu kwa safu.”

Nilisoma barua ya Shaykh Abu Bakr al-Ismaa´iyliy kwenda kwa wakazi wa Gilaan:

”Kutokana na zile khabari zilizosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni kwamba Allaah (Subhaanah) anashuka katika mbingu ya chini. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

“Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا

“… na atakapokuja Mola wako na Malaika safu kwa safu.”[2]

Tunayaamini yote hayo kama yalivyokuja pasi na kuyafanyia namna. Kama Angelitaka (Subhaanah) kutubainishia namna yake, basi Angelifanya. Kwa ajili hiyo hatusemi zaidi ya kile kilichowekwa wazi na kubainishwa na tunasimama kwa yale yasiyokuwa wazi na yenye kutatiza, jambo ambalo ndilo tumeamrishwa katika maneno Yake (´Azza wa Jall):

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

“Yeye ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu – humo mna Aayah zilizo na maana ya wazi – hizo ndio msingi wa Kitabu – na nyinginezo zisizokuwa wazi maana. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotevu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitina na kutafuta kuzipindisha, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah.”[3]

[1] 2:210

[2] 89:22

[3] 3:7

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 191-192
  • Imechapishwa: 05/12/2023