10. Ahl-us-Sunnah wanajisalimisha na Ahl-ul-Bid´ah wanaasia

Tofauti kati ya Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah, ni kwamba wanaposikia maelezo kuhusu sifa za Mola basi wanayarudisha papohapo. Hawayakubali. Au…[1] kwa dhahiri kisha baadaye wanayapindisha maana kwa lengo la kuyabatilisha maelezo kuanzia msingi wake, na kubatilisha…[2] akili na maoni yao. Hata hivyo wanajua kwa yakini kabisa ya kwamba yale aliyosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndivo kama alivosema. Kwa sababu yeye alikuwa ni mtambuzi zaidi juu ya Mola (Jalla wa ´Alaa) kuliko mwengine yeyote, na hakuna alichosema juu Yake isipokuwa ni haki, kweli na wahy. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

”Hatamki kwa matamanio yake. Hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.”[3]

Imamu wa maimamu az-Zuhriy na wengineo katika maimamu wengine (Radhiya Allaahu ´anhum) wamesema:

”Ujumbe ni wenye kutoka kwa Allaah, ni jukumu la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufikisha na jukumu letu ni kujisalimisha.”

Yuunus bin ´Abdis-Swamad bin Ma´qal amesimulia kutoka kwa baba yake aliyesema:

”al-Ja´d bin Dirham alifika kwa Wahb bin Munabbih akimuuliza kuhusu sifa Zake Allaah (Ta´ala), ambapo akasema: ”Maangamivu ni kwako, ee al-Ja´d! Kutokana na baadhi ya mambo hakika mimi nakuzingatia kuwa mwenye kuangamia. Ee al-Ja´d! Endapo Allaah asingetueleza ndani ya Kitabu Chake kwamba yuko na mikono miwili, jicho na uso, basi tusingelisema hivo. Kwa ajili hiyo mche Allaah!” Hapakupita muda mrefu kabla ya al-Ja´d kuuliwa na kusulubiwa[4].

Khaalid bin ´Abdillaah al-Qasriy, ambaye alitoa Khutbah siku ya Adhhwhaa Baswrah, akasema mwishoni mwa Khutbah yake:

“Enyi watu! Chinjeni! Allaah akubali vichinjwa vyenu. Mimi namchinja al-Ja´d bin Dirham. Kwani anadai kwamba Allaah hakumfanya Ibraahiym kuwa kipenzi wa karibu na wala hakuzungumza na Muusa maneno ya kihakika – Allaah ametakasika na kutukuka kutokana na anayoyasema al-Ja´d!”

Baada ya hapo akashuka chini, akamchinja kwa mikono yake na akaamrisha asulubiwe baada ya hapo[5].

[1] Maneno hayako wazi katika maandishi.

[2] Maneno hayako wazi katika maandishi.

[3] 53:3-4

[4] Tazama ”Siyar A´laam-in-Nubalaa’” (5/433).

[5] Tazama ”Siyar A´laam-in-Nubalaa’” (5/433).

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 189-191
  • Imechapishwa: 05/12/2023