118. Hali ilizidi kuwa mbaya katika miaka ya 200

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Katika kipindi hicho ndipo kulienea tasnifu ambayo Salaf waliita “Jahmiyyah”. Mtu ambaye yuko nyuma ya tasnifu hiyo ni Bishr al-Mariysiy na tabaka lake. Maimamu wengi, akiwemo Maalik, Sufyaan bin ´Uyaynah, Ibn-ul-Mubaarak, Abu Yuusuf, ash-Shaafi´iy, Ahmad, Ishaaq, al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw na Bishr al-Haafiy, walimsema vibaya na kumtia upotofuni.

MAELEZO

Ilipofika karne ya pili ndipo balaa likaongezeka. Ikajitokeza ´Aqiydah ya Jahmiyyah na zikatokea I´tiqaad zingine zinazopingana na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kila zama zinavyozidi kuchelewa, ndio shari huongezeka zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hautakujieni wakati wowote isipokuwa ule unaokuja baada yake ni mbaya zaidi kuliko huo mpaka mkutane na Mola wenu.”[1]

Jahmiyyah ni nisba ya Jahm bin Swafwaan, ambayo alichukua madhehebu yake kutoka kwa al-Ja´d bin Dirham. al-Ja´d bin Dirham aliyachukua madhehebu yake kutoka kwa mayahudi.

Bishr bin Ghiyyaath al-Mariysiy alikuwa ni katika Mu´tazilah na alikuwa ni mmoja wa wafuasi wa al-Ma’muun. Alikuwa na uadui na chuki dhidi ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) na alikuwa akimchochea al-Ma’muun amdhuru na ampige. Bali alimwamuru al-Ma’muun amuue na kwamba yeye atabeba jukumu la damu yake. Lakini Allaah akamlinda al-Ma’muun asifanye hivyo.

Haya makemeo ya maimamu katika kuwazungumzia vibaya hawa walioingiza katika Uislamu yale yasiyokuwa ndani yake, kama Bishr al-Mariysiy, Ahmad bin Abiy Du-aad na wengineo katika wanazuoni wa upotovu. Matahadhari dhidi yao ni mengi na yanajulikana. Haya ni katika yale ambayo Allaah huinusuru kwayo dini Yake. Watu wa haki huwajibu watu wa batili na hubatilisha shubuha zao:

كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ

”Hivyo ndivyo Allaah anavyopiga mifano.”[2]

[1] al-Bukhaariy (7068).

[2] 13:17

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 186-187
  • Imechapishwa: 07/07/2026