Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika Sunnah ni kuwakata Ahl-ul-Bid´ah na kujitenga nao mbali, kuacha mijadala na ugomvi katika dini na kutosoma vitabu vya wazushi na kutosikiliza maneno yao. Kila jambo jipya katika dini ni Bid´ah.

MAELEZO

Makusudio ya kuwakata Ahl-ul-Bid´ah ni kujitenga nao mbali, kuacha kuwapenda, kuacha kuwafanya ni marafiki, kuwasalimia, kuwatembelea na mfano wa hayo.

Kuwakata Ahl-ul-Bid´ah ni lazima. Amesema (Ta´ala):

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ

“Hutopata watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wale wanaopinzana na Allaah na Mtume Wake.”[1]

Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkata Ka´b bin Maalik na rafiki yake wakati walipoacha kwenda katika vita vya Tabuuk[2].

Lakini hapana vibaya kufanya hivo ikiwa katika kukaa nao kuna manufaa, kuwabainishia haki na kuwatahadharisha kutokamana na Bid´ah. Pengine kufanya hivo ikawa ni jambo linalotatikana. Amesema (Ta´ala):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[3]

Jambo hilo linaweza kuwa kwa kukaa nao na kuzungumza nao kama ambavyo kunaweza vilevile kukawa kwa kuwaandikia.

[1] 58:22

[2] al-Bukhaariy (4418) na Muslim (2769, 53). Rejea maneno kuhusu fiqh ya kisa hicho na zile faida na hukumu zinazopatikana ndani yake katika kitabu ”Zaad-ul-Ma´aad” (03/558) ya Ibn-ul-Qayyim.

[3] 16:125

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 158-159
  • Imechapishwa: 19/02/2023