116. Ushabiki ni wenye kusemwa vibaya

Tofauti katika mambo ya ufahamu yanatakiwa kurejeshwa katika Qur-aan na Sunnah:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[1]

Tofauti katika mambo ya ki-Fiqh yanayotokana na Ijtihaad ni jambo lisiloepukwa. Lakini mfumo wa sawa ni kurejesha tofauti hizi katika Qur-aan na Sunnah; yale yanayoafikiana na Qur-aan na Sunnah ndio ya haki na yale yanayokwenda kinyume nayo basi ni ya makosa. Kwa msemo mwingine yale ya sawa yanatakiwa kuchukuliwa na yale ya makosa yanatakiwa kuachwa. Haifai kwetu kushabikia maoni ya yeyote. Wajibu wetu ni kuyapima maoni yote katika Qur-aan na Sunnah; yale yanayoafikiana na Qur-aan na Sunnah ndio ya haki na yale yanayokwenda kinyume nayo basi ni ya makosa ingawa mwenye nayo hakukusudia kukosea. Hata hivyo maoni yake ni ya makosa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakimu akijitahidi akapatia, basi anapata ujira mara mbili, na akijitahidi akakosea, basi anapata ujira mara moja.”[2]

Analipwa thawabu kwa kujitahidi kwake na kosa ni lenye kusamehewa. Kufanya uhafidhina juu ya maoni, watu na mielekeo ndio jambo linalosimangwa na jambo la kipindi cha kale kabla ya Uislamu. Ni kitu kisichofaa. Kwa ajili hiyo ni lazima kwa muumini kuyapima maoni na matendo yake kwa Qur-aan na Sunnah. Kama ana upeo wa kufanya hivo ni vyema, vinginevyo awaulize wanachuoni ambao watambainishia ya sawa kutokamana na ya makosa. Huu ndio mfumo uliosalimika ambao Ummah huu wanatakiwa kuutendea kazi. Hakuna jengine linaloweza kuurekebisha isipokuwa hilo peke yake.

[1] 04:59

[2] al-Bukhaariy (6919) na Muslim (1716).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 89
  • Imechapishwa: 07/09/2021