Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Ni kwa nini hakusema kwamba yule mwenye kushikamana na Qur-aan, majulisho ya Qur-aan au maana ya Qur-aan au ule udhahiri wa Qur-aan katika mambo ya ´Aqiydah ni mpotofu? Ni kwa nini hakusema kuwa uongofu unapatikana kwa kule kurejea katika vipimo vya akili zenu na yale yanayozuliwa na wanafalsafa baada ya karne nne juu ya suala hili, ingawa msingi wake uliibuka mwishoni mwa zama za wanafunzi wa Maswahabah?

MAELEZO

Je, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema: “Msishikamane na dhahiri na yale yanayojulishwa na Qur-aan, kwani mwenye kushikamana nayo ni mpotevu” kama wanavyosema hawa? Kamwe. Bali alisema “Mwenye kushikamana nayo ndiye aliyenusurika:

“Ni lile litakalofuata mfano wa yale niliyomi mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

“Hakika mimi nimekuacheni kile ambacho endapo mtashikamana nacho basi hamtopotea baada yangu; Kitabu cha Allaah.”

Kwa maana nyingine Qur-aan na Sunnah.

Kwa sababu mabishano haya, kanuni hizi za mantiki na balaa hili vilitokea baada ya karne tatu au nne zilizo bora. ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu bora katika ummah wangu ni wale wa karne yangu. Kisha wale watakaowafuatia. Kisha wale watakaowafuatia. Kisha baadaye kutakuja watu wanaoshuhudia bila kuombwa kushuhudia, watakuwa makhaini na wala hawatoaminiwa, wanaweka nadhiri na wala hawatekelezi na kutadhihiri kwao unene.”

´Imraan amesema:

“Sikumbuki alisema baada ya karne yangu mara mbili au mara tatu.”[1]

Mabalaa haya yamezuka baada ya karne zilizofadhilishwa. Ni kweli kwamba baadhi yake yalitokea mwishoni mwa zama za Maswahabah na zama za wanafunzi wa Maswahabah, lakini hayakuonekana wazi. Kwa sababu Uislamu ulikuwa na nguvu. Makundi hayakuonekana isipokuwa baada ya kupita kwa karne bora wakati wa udhaifu wa waislamu.

[1] al-Bukhaariy (2651) na Muslim (2535).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 169-170
  • Imechapishwa: 06/07/2026