Allaah (Ta´ala) amesema kuwa huruma Yake umekienea kila kitu, kwamba amejilazimishia huruma juu Yake Mwenyewe na kwamba huruma Yake inashinda ghadhabu Zake. Pepo ni nyumba ya huruma Yake. Moto ni nyumba ya ghadhabu Zake.

Imethibiti namna ambavyo siku ya Qiyaamah kutaumbwa watu kwa ajili ya Pepo, watu walioanza kuingia Motoni watavyotolewa na kuingizwa Peponi na jinsi watoto watavyoingia Peponi kwa sababu ya matendo ya baba zao. Kadhalika imethibiti kuwa Peponi wataingia watu ambao kamwe hawakupatapo kufanya kheri yoyote. Imethibiti vilevile kuwa hakuna yeyote atayeadhibiwa Motoni pasi na dhambi. Huruma ya Allaah ni pana sana kiasi cha kwamba kuna kundi la wafasiri wa Qur-aan wamesema katika mnasaba wa kisa cha Fir´awn:

“Jibriyl akasema: “Ee Muhammad! Lau ungeona namna ninavyoshindilia udongo kinywani mwa Fir´awn kwa kuchelea asije kusema kitu kitachofanya Allaah akaja kumrehemu.”

Huyu ni Jibriyl, mmoja katika wajumbe wakubwa wa Malaika. Alijua jinsi huruma ya Allaah ilivyo pana. Ndipo akafanya hivo kwa kuachelea asije kurehemewa, pamoja na kuwa [Fir´awn] alisema:

أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ

“Mimi ni mola wenu mkuu.” 79:24

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 235
  • Imechapishwa: 26/12/2016