113. Yuko juu ya mbingu na ujuzi Wake umeenea kila mahali

Muqaatil bin Hayyaan (afk. 150), mwanachuoni wa Khuraasaan.

124 – ´Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal amepokea katika ”as-Sunnah” yake, kutoka kwa Nuuh bin Maymuun, kutoka kwa Bukayr bin Ma´ruuf, kutoka kwa Muqaatil bin Hayyaan, ambaye amesema kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ

“Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao.”[1]

“Yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake uko pamoja nao.”[2]

125 – al-Bayhaqiy amesimulia kutoka kwa Muqaatil bin Hayyaan ambaye amesema:

“Tumefikiwa na khabari kuhusu maneno Yake Allaah (Ta´ala) – na Allaah ndiye mjuzi zaidi:

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye karibu – Naye juu ya kila jambo ni mjuzi.”[3]

”Yeye ni wa Kwanza kabla ya kila kitu. Wa Mwisho baada ya kila kitu. Wa Dhahiri ambaye yujuu ya kila kitu. Aliyejificha ambaye yukaribu kuliko kila kitu. Ukaribu Wake ni kwa ujuzi Wake ilihali Yuko juu ya ´Arshi Yake.”[4]

Muqaatil huyu ni imamu madhubuti na alikuwa akiishi wakati wa al-Awzaa´iy. Hakuwa Ibn Sulaymaan – mzushi yule ambaye sio mwenye kuaminika.

[1] 58:7

[2] Cheni yake ya wapokezi ni nzuri. Imepokelewa katika “as-Sunnah”, uk. 71, pia katika “Masaa-il-ul-Imaam Ahmad”, uk. 263 ya Abu Daawuud, al-Laalakaa’iy (1/92/2) na al-Bayhaqiy, uk. 430-431. Imekuja katika moja ya mapokezi yake mengine kwamba Muqaatil bin Hayyaan amesimulia kwamba adh-Dhwahhaak ndiye amesema hivo. Mtunzi amesema katika ufupisho wake kwamba hayo yamethibiti kutoka kwa Muqaatil”. Imekwishatangulia katika kitabu kwa mapokezi mawili mengine.

[3] 57:3

[4] Katika cheni ya wapokezi yuko Ismaa´iyl bin Qutaybah. Ibn Abiy Haatim amemtaja Abu Sa´iyd al-Ashajj peke yake na wala hakumtajia jeruhi yoyote wala sifa. Abi Muhammad ´Abdullaah bin Muhammad bin Muusa al-Ka´biy pia amepokea kutoka kwake – mpokezi huyohuyo wa masimulizi haya kutoka kwake. Alikuwa ni katika waalimu wa al-Haakim.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 137
  • Imechapishwa: 17/07/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy