113. Tofauti ya miujiza na uchawi na kisa cha Fir´awn na Muusa

Uchawi, kwa aina zake, ni kitu kilikuwepo kwa watu tangu hapo kale. Allaah (Ta´ala) ameutaja kuhusu watu wa Fir´awn na kwamba Fir´awn alikuwa na wachawi na kati ya wananchi wake ulikuwa mwingi. Wakati Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuja na ujumbe wa Mola wake akiwa pamoja na miujiza inayofahamisha juu ya ukweli wake. Moja wapo ilikuwa ni bakora inayogeuka kuwa nyoka. Miujiza mwingine ilikuwa ni mkono wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapouingiza kwapani basi unatoka ukiwa mweupee uking´ara. Hii ni miujiza kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Sio kitu kinachoweza kutengenezwa na mtu. Mtu hawezi kufanya kitu kama hicho. Kwa sababu ni kitu kinachotoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) ambacho hukipitisha kupitia mikononi mwa Nabii au Mtume wake kwa ajili ya kumsadikisha. Amesema (Ta´ala):

وَقَالُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَاتٌ مِّن رَّبِّهِ ۖ قُلْ إِنَّمَا الْآيَاتُ عِندَ اللَّـهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ

”Wakasema: “Kwanini hakuteremshiwa alama na ishara kutoka kwa Mola wake?”  Sema: “Hakika alama na ishara ziko kwa Allaah na hakika mimi ni mwonyaji tu wa wazi.”(al-´Ankabuut 29:50)

Mtume yeye kama yeye hawezi kuleta alama na ishara isipokuwa huleta yale Allaah anampa katika miujiza.

Kuhusu uchawi ni katika matendo ya mtu yanayofanya na kuunda mtu mwenyewe na kuyamayiri. Vilevile ni katika matendo ya wa kijini na wa kibinaadamu na sio miujiza. Isipokuwa ni matendo ya kishaytwaan. Mtu anaweza kuutengeneza na kujifunza nao. Inapokuja katika miujiza hakuna yeyote awezaye kuifanya isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَقَالُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَاتٌ مِّن رَّبِّهِ ۖ قُلْ إِنَّمَا الْآيَاتُ عِندَ اللَّـهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ

”Wakasema: “Kwanini hakuteremshiwa alama na ishara kutoka kwa Mola wake?”  Sema: “Hakika alama na ishara ziko kwa Allaah na hakika mimi ni mwonyaji tu wa wazi.”

Alama na ishara zinatoka kwa Allaah. Sio kitu ambacho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaweza kukileta na kukifanya. Upande mwingine uchawi kiumbe anaweza kujifunza nao na kuufanya, japokuwa ni kitendo cha batili. Lakini miujiza ni haki. Kwa ajili hii wakati Muusa (´alayhis-Salaam) alipokuja na hoja za waziwazi na miujiza, wakasema kwamba ni uchawi na kwamba eti Muusa ni mchawi. Ndipo Fir´awn akasema:

فَلَنَأْتِيَنَّكَ بِسِحْرٍ مِّثْلِهِ

“Basi nasi tutakuletea uchawi mfano wake.” (Twaaha 20:58)

Matokeo yake akawakusanya wachawi na wakapeana ahadi na Muusa siku miongoni mwa siku na watu wakakusanyika ili wajione kitachotokea kati ya Muusa na wale wachawi. Je, wachawi watamshinda Muusa au Muusa atawashinda wachawi? Huu ni wepesi wa Allaah kwa ajili ya kudhihirisha haki na kumnusuru Mtume wake Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo wakakusanyika na wakamuomba Muusa kwamba yeye ndiye aanze kurusha vitu vyake. Lakini akawaambia wao ndio waanze. Wakarusha vile walivyonavyo na wakarusha uchawi mkubwa ambao uliwaogopesha watu na ukajaa bonde kiasi cha kwamba mpaka Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza kuogopa:

فَأَوْجَسَ فِي نَفْسِهِ خِيفَةً مُّوسَىٰ قُلْنَا لَا تَخَفْ إِنَّكَ أَنتَ الْأَعْلَىٰ وَأَلْقِ مَا فِي يَمِينِكَ تَلْقَفْ مَا صَنَعُوا

”Basi akahisi khofu katika nafsi yake Muusa. Tukasema: “Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakayeshinda na tupa kile kilichokuweko mkononi mwako wa kulia kitameza vile walivyoviunda.” (Twaaha 20:67-69)

Akairusha ile fimbo aliokuwa nayo na tahamaki ikageuka kuwa nyoka kubwa ambayo iliwaogopesha na ikameza uchawi wote waliouweka pale chini. Wao wenyewe wakaanza kuogopa juu ya nafsi zao nyola ule asije kuwameza na wao. Halafu Muusa (´alayhis-Salaam) akaizuia na bakora ile ikarudi kama ilivyokuwa. Hapo ndipo wale wachawi walitambua kuwa haya alionayo Muusa sio uchawi. Kwa sababu hii ndio sanaa na kazi yao. Wakatambua kuwa hii sio kazi ya mtu na kwamba ni kitu kutoka kwa Allaah. Ndipo wakaamini, wakatubu kwa Allaah na wakashuka chini hali ya kumsujudia Allaah (´Azza wa Jall):

وَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سَاجِدِينَ  قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ الْعَالَمِينَ  رَبِّ مُوسَىٰ وَهَارُونَ

”Wachawi wakajiangusha hali ya kusujudu wakasema: “Tumemwamini Mola wa walimwengu, Mola wa Muusa na Haaruun.” (al-A´raaf 07:120-122)

Allaah akamfedhehesha Fir´awn na wale wachawi waliokuwa upande wake katika maonyesho kama haya makubwa. Allaah akamfedhesha Fir´awn na watu wake na akayabadilisha yale waliokuwa nayo na miujiza ya kiungu ikadhihiri ambayo ndani yake haina mkono wa mtu. Wakati huo ndipo Fir´awn alipoingiwa na kiburi, akafanya ukaidi na akawatishia watu. Lakini baada ya hapo ikawa nini?

فَاقْضِ مَا أَنتَ قَاضٍ

”Hukumu unavyotaka kuhukumu.” (Twaaha 20:72-73)

 Aliwatisha kwamba atawaua na kwamba atawasulubu juu ya miti ya mitende. Lakini hata hivyo wakasubiri na wakasema:

رَبَّنَا أَفْرِغْ عَلَيْنَا صَبْرًا وَتَوَفَّنَا مُسْلِمِينَ

“Ee Mola wetu! Tujaze subira na Tufishe hali ya kuwa waislamu.” (al-A´raaf 07:126)

Mwisho mwema ukawa kwa waumini waliomuamini Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waumini. Hivyo haki ikashinda na yakasambaratika yale waliyokuwa wakiyafanya. Ikaja kubainika kwamba miujiza inayokuja na Mitume (´alayhimus-Salaam) ni katika uundaji wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hakuna mtu yeyote yule awezaye kuifanya. Si Malaika wala kiumbe mwingine. Isipokuwa ni katika uumbaji na uundaji wa Allaah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 145-147
  • Imechapishwa: 30/01/2019