Uchawi mazingaombwe au kwa msemo mwingine uchawi kiini macho, ni katika aina ile ya uchawi uliofanywa na watu wa Fir´awn  kumfanyia Muusa (´alayhis-Salaam). Pindi wachawi walikusanyika kumkabili Muusa (´alayhis-Salaam) wamuonyeshe miujiza walionayo, walifanya uchawi wa udanganyifu. Allaah (Jalla  wa ´Alaa) amesema:

فَلَمَّا أَلْقَوْا سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ

”Basi walipotupa waliyazuga macho ya watu.” (al-A´raaf 07:116)

Hakusema kwamba waliwaroga watu. Bali alisema:

فَلَمَّا أَلْقَوْا سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ وَاسْتَرْهَبُوهُمْ وَجَاءُوا بِسِحْرٍ عَظِيمٍ

”Basi walipotupa waliyazuga macho ya watu na wakawatisha na wakaja na uchawi mkubwa.” (al-A´raaf 07:116)

Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala) katika Suurah “Twaahaa”:

فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ

“Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana kwake  [yeye Muusa] kutokana na uchawi wao zinakwenda mbio.” (Twaaha 20:66)

Zikaonekana kwake kuwa zinakwenda na kutembea. Uhakika wa mambo ni kwamba zilikuwa hazitikisiki wala hazitembei. Kama ilivyo katika Aayah nyingine:

سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ

“Waliyazuga macho ya watu.”

Huu ndio uchawi wa mazingaombwe Sio uchawi wa ukweli. Uchawi kama huu unapoisha basi mambo yanarudi katika uhalisia wake. Kwa ajili hii, mchawi huja kwa baadhi ya watu na mende na vipande vya kambakamba na kuwaweka mbele yao. Wale wanaowaona wakafikiri kuwa ni wanyama.  Kisha baada ya muda wanarudi katika uhalisia wake wa hapo kabla.

Hali kadhalika wako matapeli ambao wanawajia baadhi ya watu na makaratasi ya kawaida na kuyazuga macho yao ambapo wakafikiria kuwa ni pesa. Wanabadilishana na wanachenchiwa na badala yake wanapokea pesa za kikweli mfano wake. Kisha mchawi yule anapoenda vitu hivi vinarudi kuwa katika uhalisia wake. Makaratasi yasiyokuwa na maana  yoyote. Hili ni jambo linalojulikana. Hili hutokea mara nyingi kupitia matapeli ambao wanachukua pesa za watu kwa njia ya batili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 144-145
  • Imechapishwa: 30/01/2019