111. Kitenguzi cha saba: Atakayefanya uchawi au akawa radhi nao amekufuru

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La saba:

Uchawi. Unajumuisha Swarf na ´Atwf. Atakayeufanya au akawa radhi nao amekufuru. Dalili ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

”Na [hao Malaika wawili] hawamfundishi yeyote mpaka wamwambie kwanza: “Hakika sisi ni mtihani, hivyo basi usikufuru [kwa kufanya uchawi].” (al-Baqarah 02 : 102)

MAELEZO

Uchawi – Ni ibara ya kitu kilichojificha. Kwa ajili hiyo wanachuoni wamesema kwamab uchawi ni kitu kilichojificha na ikakosekana sababu yake.

Uchawi kwa mujibu wa Shari´ah umegawanyika mafungu mawili:

La kwanza: Uchawi wa kweli.

La pili: Mazingaombwe.

Uchawi wa kweli ni kitendo kinachoathiri mwilini au moyoni. Unaathiri mwilini kwa kuugua au kwa kufa kabisa. Vilevile unaweza kuathiri katika kufikiria kwa njia ya kwamba mtu akafikiria kuwa amefanya kitu fulani ilihali ukweli wa mambo ni kwamba hajakifanya. Unaweza vilevile kuathiri kwenye moyo ambapo mtu akahisi kuchukia au kupenda kusikokuwa kwa kawaida. Hii ndio Swarf na ´Atwf. Kwa njia ya kwamba mtu akavutiwa akahisi kupenda baadhi ya vitu au baadhi ya watu kinyume na maumbile yake. Inaweza kuwa na maana vilevile ya kukichukia kitu hiki na akakibughudhi. Uchawi aina hii unatenganisha baina mke na mume. Unaitwa vilevile at-Tiwalah, kama ilivyo katika “Kitaab-ut-Tawhiyd”.

Uchawi aina ya unayaathiri macho na maono. Unaathiri kitu kinyume na uhalisia wake.

Miongoni mwa aina ya kwanza ni yale yaliyotajwa katika Suurah “al-Falaq”. Amesema (Ta´ala):

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ مِن شَرِّ مَا خَلَقَ وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَوَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ  وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ

”Sema: “Najikinga na Mola wa mapambazuko. Kutokana na shari ya alivyoviumba na kutokana na shari ya giza linapoingia na kutokana na shari ya wanaopuliza mafundoni na kutokana na shari ya hasidi anapohusudu.” (al-Falaq 113:01-05 )

Huu ndio uchawi wa kweli.

Wanaopuliza – Huyu ni yule ambaye anafunga fundo na analipulizia. Katika kufanya hivyo anakusudia kudhuru yule anayemfanyia mchawi. Kunaingia ule uchawi aliofanyiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati myahudi Labiyd bin al-A´swam alipomfanyia uchawi ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa anafikiria kuwa amefanya kitu na kumbe hakukifanya. Akaathirika kwa uchawi. Kwa kuwa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) nao ni watu. Wanasibiwa na yale yanayowasibu watu wengine katika maradhi. Miongoni mwa hayo ni maradhi. Allaah akamtumia Malaika wawili wamfanyie Ruqyah kwa Suurah hii. Mmoja wao akasema: “Mtu huyu ana nini?” Akajibu [yule Malaika mwingine]: “Amefanyiwa uchawi.” Akamuuliza tena: “Ni nani kamfanyia uchawi?” Akajibu: “Labiyb bin al-A´swam” kwenye kisima cha Dharwaan. Jibdiyl (´alayhis-Salaam) akamsomea matabano kwa Suurah hii “al-Falaq”. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasimama akiwa imara na uchawi umemwondoka. Kisha akawaamrisha watu kwenda katika kisima hiki, wauondoe uchawi huo na wauharibu. Wakamwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Si umuue?”  Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ama Allaah kishaniponya na wala sipendi kuwafungulia watu mlango wa shari.”[1]

Akawa amemwacha (SwallaAllaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuchelea kusitokee fitina. Ni dalili inayofahamisha kwamba adhabu yake alikuwa anastahiki kuuawa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema kwamba haijuzu kumuua au haistahiki kumuua. Isipokuwa alisema:

“Sipendi kuwafungulia watu mlango wa shari.”

Bi maana fitina. Kwa sababu mayahudi walikuwa na mkataba na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na lau angelimuua kungelitoa shari na fitina kutoka kwao. Hapana shaka kwamba kuzuia madhara kunatangulia kabla ya kuleta manufaa. Akawa amemuacha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuwa kikusudiwacho kimefikiwa ambacho nacho ni kupona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo hii ni aina ya uchawi wa kweli ambao unaathiri.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy (5765) na Muslim 2189 kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 142-144
  • Imechapishwa: 30/01/2019