2 – ´Amr bin ´Abasah amesema:

”Nilisema: ”Ee Mtume wa Allaah! Nikhabarisha yale aliyokufunza Allaah na ambayo mimi siyajui. Nikhabarisha kuhusu swalah.” Akasema: ”Swali swalah ya asubuhi kisha uache kuswali mpaka lichomoze jua. Kwa sababu jua huchomoza kati ya pembe ya shaytwaan, na hapo ndipo wale makafiri hulisujudia. Kisha swali, kwani hakika swalah ni yenye kushuhudia na yenye kuhudhuria mpaka mkuki upoteze kivuli chake. Kisha hapo simamisha kuswali, kwani hapo Moto unachocheka kwelikweli. Swali tena pindi kunapokuja kivuli, kwa sababu hakika swalah ni yenye kushuhudiwa na yenye kuhudhuriwa mpaka unaposwali ´Aswr. Kisha simamisha kuswali pale linapozama jua. Kwa sababu huzama kati ya pembe ya shaytwaan, na hapo ndipo hulisujudia wale makafiri.”[1]

[1] Muslim na Abu Awaanah.

Ibn Taymiyyah amesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza wakati linapochomoza jua na wakati linapozama, kwa kutoa sababu mosi ya kwamba huchomoza na kuzama kati ya pembe ya shaytwaan, pili ya kwamba hapo ndipo wale makafiri hulisujudia. Ni jambo linalotambulika ya kwamba muumini hamkusudii kumsujudia mwengine isipokuwa Allaah. Pengine watu wengi wasijue kuwa jua huchomoza na kuzama kati ya pembe ya shaytwaan na kwamba makafiri hulisujudia. Jengine ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuswali katika nyakati hizo kwa sababu ya kutojifananisha na makafiri kwa njia zote.

Hadiyth hii inatilia mkazo kwamba kila wanachokifanya washirikina katika ´ibaadah na mengineyo ambayo ima ni kufuru au maasi yaliyokusudiwa, basi muumini amekatazwa kuyafanya ingawa hakukusudia kujifananisha na makafiri. Yote haya ni kwa lengo la kufunga njia. Kwa ajili hiyo ndio maana ikakatazwa kuswali kwa kukielekea kitu kinachoabudiwa badala ya Allaah hata kama yule mfanya ´ibaadah hakukusudia jambo hilo… kwa sababu ni kujifananisha na wale wanaomsujudia asiyekuwa Allaah. Tazama jinsi Shari´ah imezikata njia zote zinazopelekea katika kujifananisha inapokuja katika mielekeo na nyakati.

Kama ambavyo wanaswali kuelekea Qiblah ambacho huswali kukielekea, basi vivyo hivyo hawaswali kuvielekea vile wanavyoswali kwa ajili yake. Bali hili la mwisho ni lenye maharibifu makubwa zaidi. Kwani Qiblah ni Shari´ah miongoni mwa Shari´ah na inaweza kutofautiana kwa kutegemea Mtume mmoja na mwengine. Kuhusu kumsujudia mwengine asiyekuwa Allaah na kumwabudu mwengine asiyekuwa Allaah ni jambo limeharamishwa ambalo Mitume wote wa Allaah wameafikiana kwalo. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَاسْأَلْ مَنْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رُّسُلِنَا أَجَعَلْنَا مِن دُونِ الرَّحْمَـٰنِ آلِهَةً يُعْبَدُونَ

“Waulize wale Tuliowatuma kabla yako miongoni mwa Mitume Wetu, je, tulifanya badala ya Mwingi wa huruma waungu wengine wakiabudiwa?” (43:45) (Iqtidhwaa’-us-Swiraat al-Mustaqiym, uk. 31)

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 170-171
  • Imechapishwa: 01/11/2023