110. Hakuna nukuu hata moja juu ya ufahamu wa kimafumbo

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Ni vipi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala yeyote katika Salaf hatajapatapo siku hata moja kusema kwamba hatutakiwi kuamini yale ambayo yanafahamishwa na Aayah na Hadiyth hizi? Ni kwa nini hawakutuamrisha kuamini yale ambayo akili zetu zinapelekea kwayo au tuamini hili na lile? Kwa sababu haki inapatikana katika ule uinje wake. Yachunguzeni na myakubali yale yanayoafikiana na vipimo vya akili zenu na yale yasiyokuwa hivo basi ima yakalieni kimya au yakataeni!

MAELEZO

Si Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Salaf hawajapatapo kusema kuwa Aayah hizi kuhusu majina, sifa za Allaah na Tawhiyd kwamba haziko katika udhahiri wake na hivyo msiziamini. Bali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametufunza Qur-aan na akatufikishia nayo bila kututahadharisha kuijengea hoja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametufunza Qur-aan na akatufikishia nayo. Allaah amemwamrisha kuwafikishia nayo watu:

وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ

“Nimefunuliwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itakayomfikia.”[1]

Salaf waliisoma Qur-aan. Haikuwatatiza. Hawakuchukua msimamo wa kunyamaza juu ya Aayah yoyote. Jambo likiwatatiza, basi wanakirudisha kile kisichokuwa wazi kwa kile kilicho wazi, wanafasiri kile kisichokuwa wazi kwa kile kilicho wazi. Kwa sababu maneno ya Allaah hayagongani. Baadhi yanafasiri mengine. Ikiwa kuna ambaye hajui namna atakavyojengea Qur-aan dalili, basi awaulize wanazuoni:

فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.”[2]

Huu ndio mfumo wa Salaf. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hajapatapo kutwambia tusiamini kile alichotueleza ndani ya Qur-aan hii. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hajapatapo kutwambia tusiamini kile alichotueleza ndani ya Sunnah. Salaf, wakiwemo Muhaajiruun, Answaar, wanafunzi wa Maswahabah na wanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah, hakuna yeyote katika wao aliyewahi kuchukua msimamo wa kuzinyamazia Aayah hizi. Walizisoma, wakaamini yale yanayofahamishwa nazo na wakazifasiri. Hazikuwababaisha. Baadaye eti wanajitokeza watu na mfumo mpya, wanapingana na yale yanayojulishwa na Qur-aan, Sunnah na Salaf, na kuwaambia watu eti huo ndio mwongozo.

Allaah hajapatapo kusema tuamini tu yale yanayofahamishwa na kuafikiana na akili zetu. Isitoshe viwango vya akili ni mantiki, mijadala na falsafa. Allaah hajapatapo kusema tusiamini yale yanayopingana na akili yetu kutokana na udhahiri wake na kwamba badala yake tuyapindishe kutokana na udhahiri wake. Huu ndio mfumo wao. Yale ambayo Qur-aan inaafikiana na akili zao, wanayakubali, na yale ambayo yanapingana na akili yao, basi hawayatendei kazi na badala yake wanaifanyia kazi akili yao. Ima Qur-aan waipindishe maana kutokana na udhahiri wake au wanadai kuwa wanaitegemeza maana yake kwa Allaah. Wao ima ni wenye kuipindisha maana au wenye kuitegemeza maana yake. Huu ndio mwenendo wa wale waliokuja nyuma. Aidha wanasema kuwa mfumo wao ndio mjuzi na wenye hekima zaidi kuliko mfumo wa Salaf.

[1] 6:19

[2] 16:43

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 162-164
  • Imechapishwa: 09/09/2024