11. Sharti ya kumi ya wudhuu´ ni kuingia wakati kwa mtu ambaye hadathi yake ni ya daima

Sharti ya kumi ni kuingia wakati wa swalah ya faradhi kwa yule mtu ambaye hadathi yake ni yenye kudumu. Maana yake ni kwamba mtu ambaye anatokwa hovyo na mkojo, anatokwa na upepo bila kukoma na pia mwanamke mwenye damu ya ugonjwa, hawa wote ni lazima watie wudhuu´ kila mara wakati wa swalah ya faradhi unapowadia. Hivyo akitawadha mmoja wao kwa ajili ya swalah ya Dhuhr baada ya kuingia wakati wake na akaiswali, kisha ukafika wakati wa swalah ya ´Aswr, basi haifai akaswali ´Aswr kwa wudhuu´ wa Dhuhr. Ni lazima aweke wudhuu´ mpya baada ya kuingia wakati wa ´Aswr. Dalili ya hili ni amri yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Faatwimah bint Abiy Hubaysh (Radhiya Allaahu ´anh) – aliyekuwa na damu ya ugonjwa – atawadhe kwa ajili ya kila swalah. Ameipokea al-Bukhaariy (228) kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 12
  • Imechapishwa: 04/05/2026