11. Ni ipi hukumu ya kunyoa ndevu au kuzikata na ni upi mpaka wake?

Swali 11: Ni ipi hukumu ya kunyoa ndevu au kuzikata na ni upi mpaka wake?

Jibu: Kunyoa ndevu ni haramu kwa sababu mtu anajifananisha na washirikina na waabudia moto. Mtume (Swalla Alaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”[1]

Aidha ni kubadilisha maumbile ya Allaah na kufuata maamrisho ya shaytwaan. Allaah (Subhaanah) amesema juu yake:

وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ

“Nitawaamrisha watabadili uumbaji wa Allaah.”[2]

Jengine ni kwamba mtu anaondosha yale maumbile ambayo Allaah amemuumba juu yake. Kuachia ndevu ni katika maumbile. Kadhalika ni kwenda kinyume na mwongozo wa waja wema wa Allaah ambao ni Manabii, Mitume na wale wafuasi wao. Ndevu zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zilikuwa nyeupe na nyingi na Allaah (Ta´ala) akaeleza kuwa Haaruun alimwambia ndugu yake Muusa (´alayhimaas-Salaam):

يَا ابْنَ أُمَّ لَا تَأْخُذْ بِلِحْيَتِي وَلَا بِرَأْسِي

“Ee mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu na wala kichwa changu.”[3]

Kwa hivyo kuzinyoa ni kutoka nje ya mwongozo wa waja wema wa Allaah ambao ni Manabii, Mitume na wengineo.

Kuzikata ni kuasi amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye alisema:

“Na ziacheni ndevu zikuwe.”[4]

“Fugeni ndevu.”

Inajulisha kuwa mwenye kupunguza kitu anakuwa amemuasi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na ambaye amemuasi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi amemuasi vilevile Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ

“Atakayemtii Mtume, basi kwa hakika amemtii Allaah.”[5]

وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

“Anayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika amepotoka upotofu wa wazi.”[6]

Utashangazwa na watu ambao wanasema kuwa kunyoa ndevu inafaa, licha ya kuwa wanajua kuwa ni katika desturi za waislamu, mwongozo wa Mitume na kujua kwao amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuziacha zikuwe. Licha ya hivo wanasema kuwa inafaa na kwenda kinyume na njia ya waumini.

Kwa mujibu wa maneno ya watu wa lugha mpaka wa ndevu ni nywele za kwenye kidevu na mashavuni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Na ziacheni ndevu zikuwe.”

Neno “na” halikuziwekea ndevu mpaka kwa mujibu wa Shari´ah. Wakati yanapokuja maandiko pasi na mpaka uliowekwa katika Shari´ah, basi jambo hilo litachukuliwa kwa mujibu wa mpaka wa watu wa lugha, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anazungumza kwa lugha ya kiarabu na Qur-aan iko kwa kiarabu.

[1] Ahmad na Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri.

[2] 04:119

[3] 20:94

[4] al-Bukhaariy na wengineo.

[5] 04:80

[6] 33:36

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 01/03/2023