11. Mtendaji upande wa jina, si mtendaji upande wa uhakika

Kuhusu Sunnah, Rifaa´ah bin Raafiy´ ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia mbedui aliyekuwa anaswali kwa haraka:

“Rejea uswali; kwani hakika hujaswali.”[1]

Bwana yule akarudi tena na tena, kila akirudi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anamwambia tena:

“Rejea uswali; kwani hakika hujaswali.”

Alisema hivo ilihali amemuona akiswali. Huoni kuwa ameswali kwa upande wa jina lakini hajaswali kwa upande wa uhakika? Vivyo hivyo kuhusu mwanamke anayemuasi mume wake, mtumwa aliyetoroka na mtu anayewaswalisha maamuma wanaomchukia; swalah zao hazikubaliwi[2].

Mfano mwingine ni Hadiyth ya ´Abdullaah bin ´Umar kuhusu mwenye kunywa pombe kwamba swalah zake hazitokubaliwa kwa nyusiku arobaini[3].

Vilevile ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Hana swalah ambaye anaishi jirani na msikiti isipokuwa msikitini.”[4]

Hadiyth ya ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) inayosema kuhusu mwenye kutuma mzigo wake usiku wa 12 Dhul-Hijjah:

“Hana haji yoyote.”

Hudhayfah amesema:

“Yule mwenye kufikiria muonekana wa mwanamke aliye uchi ilihali amefunga, ameiharibu swawm yake.”[5]

Aathaar zote hizi na mfano wake maana yake ni vile nilivyokufasiria.

[1] Hadiyth imesimuliwa na Rifaa´ah bin Raafiy´ az-Zarqiy. Ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Imetajwa katika kitabu ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (337). al-Bukhaariy na Muslim wameipokea kupitia kwa Abu Hurayrah.

[2] Ibn Maajah, Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” na adh-Dhwiyaa’ katika ”al-Mukhtaarah” kupitia kwa Ibn ´Abbaas. Hadiyth inasema:

“Allaah hazikubali swalah za watu watatu: imamu anayewaswalisha watu ilihali wanamchukia…”

Inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Abu Umaamah ambayo at-Tirmidhiy ameifanya kuwa nzuri.

[3] Ahmad (3/35) kupitia kwa Ibn ´Umar, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Mwenye kunywa pombe basi swalah zake hazitokubaliwa kwa nyusiku arobaini.”

Wapokezi wake ni waaminifu. Hadiyth ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy. Ahmad (2/197) pia ameipokea kupitia kwa Ibn ´Umar kwa cheni ya wapokezi Swahiyh iliyosahihishwa na Ibn Hibbaan.

[4] Haya hayasihi kutoka kwa ´Aliy. Ameyapokea al-Haarith bin al-A´war ambaye ameachwa. ad-Daaraqutwniy pia amepokea mfano wake kupitia kwa Jaabir na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhum).  Hiyo pia si Swahiyh.

[5] Imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo imezuliwa, kama ilivyotajwa katika ”al-Laaliy al-Masnuu´ah” ya as-Suyuutwiy.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 82-85
  • Imechapishwa: 04/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy