11. Makafiri waliopigwa vita walikuwa wanakubali Tawhiyd-ur-Rububiyyah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa kwanza utambue kuwa makafiri ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita, walikuwa wakikubali ya kwamba Allaah (Ta´ala) ndiye Muumbaji Mwenye kuyaendesha mambo. Hata hivyo hili halikuwaingiza wao katika Uislamu. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُون

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa [aliye] hai kutoka maiti na anayemtoa maiti kutoka [aliye] uhai na nani anayeendesha mambo? Watasema: “Ni Allaah”. Basi sema: “Je, basi hamchi?”[1]

MAELEZO

Utambue kuwa wale makafiri ambao Mtume wa Allaah aliwapiga vita, akahalalisha kuuliwa na akahalalisha mali zao walikuwa wakikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na kwamba Allaah ndiye Mwenye kuumba, Mwenye kuruzuku na Mwenye kuyaendesha mambo. Hata hivyo akahalalisha kuuliwa na akawakufurisha. Hii ndio inaitwa Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ambayo ni kule kumpwekesha Allaah katika matendo Yake. Kumpwekesha Allaah katika matendo Yake kukiwemo uumbaji, uruzukaji, kufisha, kuhuisha na matendo Yake mengine (Subhaanah).

Zipo Aayah nyingi zinazoonyesha kuwa makafiri walikuwa wakikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Miongoni mwazo ni zifuatazo:

1 – Maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

”Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye hai na nani anayeendesha mambo?”  Watasema: “Ni Allaah”, basi sema: ”Je, basi kwa nini hamchi?”[2]

2 – Maneno Yake (Ta´ala):

قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ

”Sema: ”Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo humo mkiwa mnajua?” Watasema: ”Ni ya Allaah.” Sema: ”Je, basi hamkumbuki?” Sema: ”Nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ‘Arshi kuu?” Watesema: ”Ni ya Allaah.” Sema: ”Je, basi kwa nini hamchi?” Sema: ”Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu, Naye ndiye alindaye na wala hakilindwi chochote kinyume Naye, ikiwa mnajua?” Watasema: ”Ni Allaah pekee.” Sema: ”Basi vipi mnazugwa?”[3]

3 – Maneno Yake (Ta´ala):

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ فَأَنَّى يُؤْفَكُونَ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.” Basi ni wapi wanakogeuziwa!”[4]

Makafiri wa Quraysh wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah licha ya hivyo hawakuingia ndani ya Uislamu. Sababu ni kwa kuwa walipinga Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee ikiwa ni pamoja na kumuomba du´aa, kuchinja, kuweka nadhiri na nyinginezo. Walimshirikisha Yeye na wengine. Walimchinjia Allaah na wakawachinjia wengine, wakamuwekea nadhiri Allaah na wakawawekea nadhiri wengine, wakamuomba Allaah na wakawaomba wengine, jambo ambalo ndio shirki. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakufurisha, akawapiga vita na akahalalisha kuuliwa na kuchukua mali zao licha ya kwamba wanakiri Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah.

[1] 10:31

[2] 10:31

[3] 23:84-89

[4] 43:87

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 131-132
  • Imechapishwa: 05/03/2023