Lengo la kumi na moja: Kukumbuka Aakhirah

Miongoni mwa malengo makubwa ya hajj ni kukumbuka Aakhirah na kukumbuka kusimama mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Zingatia kitu cha kwanza anachoanza nacho muislamu katika matendo yake ya hajj wakati anapovua mapambo yake, mavazi yake na hali aliyoizowea. Kila mwenye kuhiji amezowea katika nchi yake kuvaa vazi la aina fulani. Utawaona wote wanapofika katika Miyqaat wanavua nguo zao zilizoshonewa, wanaoga na wanajitia manukato. Kisha wote hao wanavaa Izaar na Ridaa´ nyeupe na safi. Izaar ambayo anaizungusha katika nusu ya sehemu ya mwili wake kwa chini. Ridaa´ anaiweka katika mabega yake. Namna hii ya unyenyekevu na sifa hii ambayo inawasawazisha wote; tajiri na masikini, raisi na raia, kiongozi na yule mwenye kuongozwa, mdogo na mkubwa, wote wanakuwa sawa katika hayo.

Muonekano huu ambao unawasawazisha wote pindi wanapokuwa ni wenye kuelekea katika Nyumba ya Allaah ndivo watavokuwa sawa wakati watapoyaacha maisha haya. Hamuwaoni wale wanaokufa huenda na nini kutoka katika dunia hii? Huingia ndani ya kaburi akiwa na kitu gani? Hakuna anachoingia nacho ndani ya kaburi isipokuwa ni vipande vya vitambara vilivyozungushwa katika mwili wake, akaswaliwa baada ya kuoshwa kisha akaingizwa ndani ya kaburi lake. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam:

“Watafufuliwa watu siku ya Qiyaamah wakiwa uchi, peku, pasi na kutahiriwa na wakiwa hawana chochote.” Tukauliza: “Nini maana ya Buhmaa?” Akasema: “Watakuwa hawana chochote.”[1]

Hakuna mashamba, biashara, mali, uongozi wala kitu kingine. Kwa hivyo vazi la Ihraam linamkumbusha mtu vazi la sanda.

Kusimama katika uwanja wa ´Arafah kunamkumbusha mtu kusimama mbele ya Allaah (´Azza wa Jall) siku ya Qiyaamah. Zingatia namna ambavyo viumbe wote ulimwenguni watakusanyika katika uwanja mmoja na katika kipindi kimoja. Ni nani ambaye amewakusanya mkusanyo huu? Ni Mola wa walimwengu ambaye atawakusanya wa mwanzo na wa mwisho katika uwanja mmoja siku ya Qiyaamah. Atawakusanya wote, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho, aliyekufa kwa kuungua na moto, aliyeliwa na wanyama na akatoka kwa yule mnyama akiwa ni kinyesi, aliyezikwa na akapotea chini ya udongo:

وَقَالُوا أَإِذَا ضَلَلْنَا فِي الْأَرْضِ أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ

“Wakasema: “Je, tutakapopotea chini ya ardhi, je, hivi kweli sisi tutaumbwa katika umbo jipya tena?”[2]

Wote hawa watakusanywa na Mola wa walimwengu. Kusimama kwako ´Arafah kunakukumbusha kusimama kwako mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) siku ya Qiyaamah.

Imethibiti katika “al-Musnad” ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwaambia watu kabla ya kutua kwa jua ilihali amesimama ´Arafah:

“Enyi watu! Hakika haikubakia katika dunia yenu isipokuwa ni mfano wa kile kilichobakia katika siku yenu hii.”[3]

Mahujaji wanasimama katika kiwanja cha ´Arafah. Kila mmoja katika wao anataraji kuachiwa huru na Moto katika siku kama hiyo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna siku ambayo Allaah humwacha mja huru na Moto kama siku ya ´Arafah.”[4]

Siku ambayo Allaah huwaacha huru watu wengi na Moto ni siku ya ´Arafah. Kwa ajili hii inatakikana matumaini ya muislamu katika siku hii yawe ni yenye nguvu ili aachwe huru na Moto na atoke katika uwanja wa ´Arafah na huku ameachwa huru na Moto. Ee Allaah! Tuache huru; sisi, baba zetu, kizazi chetu na wake zetu, kutokamana na Moto, ee Mola wa walimwengu.

Katika hajj kuna nembo kubwa za hajj na sehemu nyingi tukufu za kusimama zinazomkumbusha mtu kufufuliwa, malipo, hesabu na kusimama mbele ya Allaah (Subhaanah) siku ya Qiyaamah. Kwa ajili hii zingatia, ee mwenye kuhiji, Aayah za hajj katika Suurah “al-Baqarah” zimemalizika vipi? Amesema (Ta´ala):

فَمَن تَعَجَّلَ فِي يَوْمَيْنِ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ وَمَن تَأَخَّرَ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ ۚ لِمَنِ اتَّقَىٰ ۗ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ

“Atakayeharakisha kuondoka katika siku mbili, basi si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa yule mwenye kuogopa. Mcheni Allaah na tambueni kwamba Kwake mtakusanywa.”[5]

Hili ni jambo unalotakiwa kulichukua na kwenda nalo unapomaliza hajj yako na urudi katika mji wako ukiwa nalo:

وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ

“Mcheni Allaah na tambueni kwamba Kwake mtakusanywa.”

Kwa sababu hajj inakukumbusha kufufuliwa, malipo na hesabu. Kwa hivyo, ewe ambaye umehiji Nyumba ya Allaah, mche Allaah! Kumbuka kuwa utafufuliwa mbele ya Allaah na kwamba Allaah atakufanyia hesabu na kukulipa kwa yale uliyotanguliza katika maisha haya.

Tambua kuwa maisha haya ya dunia ni yenye kutupa mgongo na kwamba Aakhirah ndio yenye kutukabali na kwamba kila mmoja katika wao ana wana. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuweni katika wana wa Aakhirah na msiwe katika wana wa dunia. Hakika hii leo ni matendo na hakuna hesabu na kesho ni hesabu hakuna matendo.”

Mja akiwa na utambuzi, elimu na yakini hii ya kwamba atakusanywa na Allaah, basi elimu na yakini yake hii itakuwa ni yenye kumsaidia katika kuyatengeneza matendo yake na kujiandaa kwa ajili ya siku hiyo. Allaah amesema katikati ya Aayah za hajj:

وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ ۚ وَاتَّقُونِ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ

“Chukueni masurufu. Hakika bora ya masurufu ni kumcha Allaah. Nicheni Mimi, enyi wenye akili.”[6]

Yule ambaye yuko juu ya yakini ya kukusanywa, kulipwa na kufanyiwa hesabu basi yakini yake hii inakuwa ni yenye kumsaidia katika kuyatengeneza matendo yake:

قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ

“Watasema: “Hakika sisi tulikuwa hapo kabla kwenye familia zetu wenye kuogopa.”[7]

Bi maana tulikuwa na khofu ya kufufuliwa, kukusanywa, kulipwa na kusimama mbele ya Allaah. Khofu hii ndio imetufanya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

فَمَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ

“Basi Allaah akatuneemesha na akatuokoa na adhabu ya Moto unaobabua.”[8]

Yule ambaye atapewa kitabu chake kwa mkono wa kuume atasema siku ya Qiyaamah:

إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ

“Hakika mimi nilikuwa na yakini kuwa hakiki mimi ni mwenye kukutana na hesabu yangu.”[9]

Bi maana nilikuwa nikiamini na kuyakinisha kwamba kuna siku ya kufufuliwa, ya kufanyiwa hesabu na ya kukusanywa. Matokeo yake nikawa ni mwenye kujiandaa kwa ajili ya siku hiyo.

[1] Ahmad katika ”al-Musnad” (16042) na al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (3638).

[2] 32:10

[3] (6173).

[4] Muslim (1348).

[5] 02:203

[6] 02:197

[7] 52:26

[8] 52:27

[9] 69:20

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 55-61
  • Imechapishwa: 22/08/2018