Lengo la kumi: Kuwakhalifu washirikina

Miongoni mwa malengo ya hajj ni kwenda kinyume na washirikina katika matendo yao, upotevu wao, ujinga wao na batili yao isiyokuwa na kiwango wala isiyohesabika. Kwa ajili hiyo ndio maana tunamuona Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakhalifu washirikina katika matendo yao ya hajj. Walikuwa wakihiji, wakifanya Talbiyah, wakisimama ´Arafah na wakisimama Muzdalifah. Lakini pamoja na yote haya walikuwa katika upotevu wa upofu na ujinga mkubwa kabisa. Talbiyah yao ilikuwa imejengwa juu ya shirki na kumfanyia Allaah washirika. Mmoja katika wao alikuwa anasema katika Talbiyah yake:

“Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia, huna mshirika Wewe, isipokuwa mshirika Wako ambaye unammiliki na anavyomiliki.”

Wanachanganya katika Talbiyah kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) na kumfanyia washirika. Hii ndio maana ya maneno ya Allaah pale alipobainisha hali yao:

مَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ

“Wengi kati yao hawamuamini Allaah isipokuwa wao ni wenye kufanya shirki.”[1]

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

”Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatangaza Tawhiyd. Washirikina katika hajj yao walikuwa wakitoka ´Arafah kabla ya kutua kwa jua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajitofautisha nao na akafanya kutoka ´Arafah ni baada ya kuzama kwa jua. Walikuwa pia wanatoka Muzdalifah baada ya jua kutua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajitofautisha nao na akatoka hapo baada ya jua kupiga wekundu na kabla ya jua kuchomoza. Yote haya kwa ajili (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwakhalifu washirikina. Walikuwa hawaoni kufaa kufanya ´Umrah katika miezi ya hajj. Bali wakichukulia kufanya hivo katika miezi hiyo ni katika uovu mkubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaenda kinyume nao na ´Umrah zake zote akazifanya katika miezi ya hajj. Vivyo hivyo matendo na ´ibaadah zengine za hajj zinazofanywa na muislamu zinapaswa kusalimika kutokamana na upotevu wa watu wa kipindi cha ukafiri na upumbavu wa watu wa batili. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowakhutubia watu katika hajj alisema katika Khutbah yake:

“Kila jambo katika mambo ya kipindi cha kikafiri nimeyaweka chini ya miguu yangu na kuyakanyaga. Damu za kipindi cha kikafiri imekwisha. Damu ya kwanza ninayoiangusha katika damu zetu ni damu ya Ibn Rabiy´ah bin al-Haarith. Alikuwa amepelekwa kwa Banuu Sa´d anyonyeshwe ambapo Hudhayl akamuua. Ribaa ya kipindi cha kikafiri imekwisha. Ribaa ya kwanza ninayoiangusha ni ribaa yetu ambayo ni ya ´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib. Zote naziangusha.”[3]

Katika haya ndani yake kuna ubainifu wa hali duni na ufisadi mkubwa waliokuwemo watu kabla ya kuja Uislamu katika ´ibaadah zao na matangamano yao. Damu ilikuwa ni yenye kumwagwa hovyo, mali inakiukwa na heshima inavunjwa kutokana na ujinga na upotevu ulivyokuwa umefikia kilele. Kwa ajili hiyo wakapata hasira na ghadhabu za Allaah (´Azza wa Jall).

Kwa hivyo muislamu anatakiwa kufaidika na hajj yake kuhakikisha kuwakhalifu maadui wa dini ya Allaah (Subhaanah), awe ni mwenye kujifakhari na dini yake na atahadhari kwelikweli kujifananisha na maadui wa Allaah. Anatakiwa kutambua nafasi ya neema hii. Achunge nafasi ilionayo hali ya kuitengeneza nafsi yake mwenyewe na kuitengeneza jamii. Sambamba na hilo awe ni mwenye kufuata mienendo na njia ya Uisamu ilionyooka. Vilevile atahadhari kwelikweli kutokamana na matendo ya kipindi cha kikafiri, upumbavu wake na upotevu wake. Yote haya ili aweze kupata radhi na rehema za Allaah. Yote haya ili aweze kusalimika na hasira na ghadhabu za Allaah. Imethibiti katika Hadiyth ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu wanaochukiwa zaidi na Allaah ni aina tatu; mwenye kufanya uovu katika Haram, mwenye kutaka [kuingiza] katika Uislamu mwenendo wa kipindi cha kikafiri na mwenye kutaka kuimwaga damu ya mtu pasi na haki.”[4]

Hakika katika msiba na balaa kubwa ni kwamba utaona kwa watu wengi wameichukulia wepesi dini yao. Hayo yatapata kudhihiri kwao pindi wanapozungumza na makafiri na kujifananisha nao. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu; hatua kwa hatua, shibiri kwa shibiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia.”[5]

Aliyasema hayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuutahadharisha Ummah wake wasije kufuata kipindi cha kikafiri na kufuata mienendo ya makafiri na washirikina.

Shimo la mburukenge liko tofauti na mashimo ya wanyama wengine wanaotambaa kwa njia ya kwamba kule shimoni kuna konakona kiasi cha kwamba mtu akitaka kumkamata basi hawezi kumpata kutokana na namna lilivyopindapinda sana. Hii maana yake ni kwamba iwapo makafiri watafanya matendo yaliyopinda kabisa, basi watapatikana katika waislamu ambao watawaiga. Hapa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaelezea juu ya jambo la makadirio na mipango ya kilimwengu iliopangwa na Allaah kwamba litatokea na wakati huohuo ndani yake mna matahadharisho. Bali mtindo kama huu ni kutahadharisha kwa khatari zaidi. Anaelezea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba litatokea kwa sababu Allaah amelipanga na kulikadiria. Ndani yake kuna matahadharisho kutokamana na kitendo hicho. Kwa hiyo muislamu atahadhari sana. Imekuja katika Hadiyth:

“Mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”[6]

Lililo la wajibu kwa kila muislamu aliyeisikia Hadiyth hii na ikaingia ndani ya moyo wake atahadhari kwelikweli kuwaigiza makafiri na kujifananisha na maadui wa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Jambo hilo linatiliwa mkazo zaidi khaswa katika wakati kama huu ambapo watu wamefunguka zaidi katika kuiga desturi za makafiri na kufuata matendo yao kwa kiasi kikubwa kabisa. Majumba ya waislamu yamekuwa yanafikiwa na tamaduni za makafiri – bali upumbavu wao – ndani kabisa ya majumba yao kupitia chaneli hizi za TV, intaneti na magazeti mabaya. Matokeo yake fikira zinabadilika, akili zinaharibika na dini inayumbishwa, tabia inaharibiwa na watu wanatumbukia katika aina mbalimbali ya kujifananisha na maadui wa dini ya Allaah. Khaswakhaswa katika safu ya vijana wengi wa Kiislamu, wakiume na wakike, yote haya kwa sababu ya ujinga na kujiweka mbali na dini ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). at-Twabariy amepokea katika “Tahdhiyb-ul-Aathaar”  kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Zitawajia watu zama ambazo nyoyo zitakuwa za waajemi.”[7]

Makusudio ya waajemi ni maadui wa dini ya Allaah katika mayahudi, manaswara na wengineo katika viongozi wa ukafiri na upotevu. Zitawajia watu zama ambazo nyoyo zitakuwa za waajemi kwa sababu ya kutotaka kujifunza dini ya Allaah, ujinga mwingi, kipindi hicho nyoyo zitakuwa zimeelekea kujifananisha na makafiri, kuwafuata kichwa mchunga katika sherehe zao, desturi zao, mavazi yao na mambo yao mengine. Hii ni hali mbovu ambayo muislamu anayejipendelea kheri juu ya nafsi yake anatakiwa kujilinda na Allaah kutokamana na hali kama hii – Allaah atukinge sote kufuata njia ya wale walioghadhibikiwa na waliopotea.

[1] 12:106

[2] 02:22

[3] Muslim (1218).

[4] al-Bukhaariy (6882) kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[5] al-Bukhaariy (7320), Muslim (2669), Ahmad katika ”al-Musnad” yake (8340) na tamko ni lake.

[6] Ahmad (5115).

[7] (201) kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Tazama ”as-Swahiyhah” (3357) ya al-Albaaniy.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 48-55
  • Imechapishwa: 22/08/2018