Lengo la kumi na mbili: Kuhakikisha udugu wa kidini

Miongoni mwa malengo makubwa ya hajj ni kuhakikisha udugu wa kidini na mafungamano ya kiimani. Undugu huu unadhihiri wakati wa hajj na kuwa wazi katika sura yake ilio nzuri na pambo lake lililo tukufu zaidi. Mahujaji hawa wanakusanyika katika uwanja wa ´Arafah na wanakusanyika katika Muzdalifah ambapo wote nguo yao ni moja, lengo lao ni moja, mwabudiwa Wao ni mmoja, matendo yao ni mamoja, Qiblah chao ni kimoja, wanayemfuata ni mtu mmoja ambaye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanashirikiana katika matarajio na maumvivu. Matarajio yao ni mamoja. Maumivu yao ni mamoja. Hamu yao ni zenye kushirikiana. Wamekusanyika katika mkusanyiko mkubwa wa Kiislamu ambao unaonyesha mafungamano ya kiimani na udugu wa kidini. Utamuona mmoja ni mwekundu. Mwingine ni mweusi. Mmoja ni mwarabu. Mwingine si mwarabu. Wote hao kilichowakusanya ni dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna tofauti kati ya wote hao isipokuwa kwa kumcha Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ

“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke na tukakufanyeni kuwa mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye mbora zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni yule mwenye taqwa zaidi kati yenu. Hakika Allaah ni Mjuzi, Mwenye khabari zote.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj ya kuaga:

“Enyi watu! Tanabahini! Hakika Mola wenu ni mmoja. Baba yenu ni mmoja. Hakuna fadhilah kwa mwarabu juu ya asiyekuwa mwarabu, asiyekuwa mwarabu juu ya mwarabu, wala mwekundu juu ya mweusi wala mweusi juu ya mwekundu isipokuwa kwa kumcha Allaah. Je, nimefikisha?” Wakasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefikisha.”[2]

Hajj ni mafungamano makubwa ambayo yanawakusanya watu wa imani katika umoja, kupendana, kusaidiana katika wema na uchaji, kutekeleza maamrisho ya Allaah (´Azza wa Jall) na kuwaangalia mafukara. Yatazame hayo kupitia zile zawadi na fidia/kafara zinazotolewa katika hajj wakati yule mwenye kuhiji anapofanya upungufu katika matendo ya hajj ambayo ni ya wajibu na akafanya makatazo katika makatazo ya hajj. Tazama namna ambavyo haya yanawanufaisha wale mafukara kiasi kikubwa na yakawafaidisha faida kubwa. Katika hajj udugu, kushikamana na kusaidiana katika wema na kumcha Allaah, ni mambo ambayo yanapata kuonekana.

Katika siku hii tukufu, siku ya ´Arafah, mahujaji wanasema “Laa ilaaha illa Allaah” kwa wingi. Ndio kitu bora kinachoweza kusemwa katika siku kama hii. Bali ndio neno bora zaidi kabisa na linalopendwa zaidi na Allaah. Imethibiti katika Hadiyth ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Du´aa bora ni du´aa ya siku ya ´Arafah. Bora niliyosema mimi na Mitume wengine kabla yangu: “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa pekee hana mshirika. Ufalme ni Wake, himdi ni Zake Naye juu ya kila jambo ni muweza.”

Katika haya kuna ishara kubwa inayoonyesha kwamba kukusanyika kwa waislamu hakukuwi isipokuwa juu ya Tawhiyd na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani jambo hilo ndilo linalotokomeza matamanio, kuondosha uadui, chuki, kuzikutanisha nyoyo na kuleta umoja. Kila ambavyo watadhoofika katika kushikamana na neno hili ndivyo utavyodhoofika umoja na mshikamano wao kutegemea na udhaifu walonao.

Halafu huu msakunyiko mkubwa wa watu ambao rangi zao ni tofauti, ndimi zao ni tofauti, wanatoka nchi mbalimbali na wote wamekusanyika katika makusudio na lengo moja linapata kudhihiri kupitia neno hili wanalolitamka na kulirudirudi. Kilichowakusanya ni Tawhiyd ya Allaah na kumuamini. Kilichowaunganisha ni kumnyenyekea Allaah na kudhalilika mbele Yake hali ya kuwa ni wenye shauku na woga, matarajio na khofu na kwa kupenda na kutumai. Kwa hivyo neno la Tawhiyd “Laa ilaaha illa Allaah” ndio mafungamano ya kikweli ambayo wamekusanyika juu yake waislamu. Wanapenda kwa ajili yake. Wanajenga uadui kwa ajili yake. Wanapenda na kubughudhi kwa ajili yake. Kwa ajili yake jamii ya Kiislamu imekuwa kama kiwiliwili kimoja na kama jengo lililoshikana; upande mmoja unaupa nguvu upande mwingine.

Miongoni mwa malengo makubwa ya hajj ni kuyafanya mafungamano na uhusiano huu kuwa na nguvu. Mola anayeabudiwa ni mmoja. Qiblah kinachoelekewa ni kimoja. Mtume anayefuatwa ni mmoja. Vazi la Ihraam, nembo za hajj na matendo yake ni mamoja. Sehemu wanayokusanyika waislamu na wakati wake ni mmoja. Kauli mbiu ya kila mmoja ni “Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia” hali ya unyenyekevu na udhalilikaji. Hivi kweli kuna mafungamano yenye nguvu kuliko haya? Hivi kweli kuna uhusiano wenye nguvu kuliko uhusiano huu?

Zinduka! Waislamu wanatakiwa kuyafahamu hayo. Wanatakiwa kumshukuru Allaah kwa muafikiano huu uliobarikiwa na mkarimu, mapenzi na udugu. Kila mmoja katika wao ajitahidi kufanya kile ambacho kinautia nguvu na kuukuza udugu huu. Sambamba na hilo wajiepushe na kila jambo linaloudhoofisha. Kila mmoja aweke kando mambo ya kasumba, ya uinchi, mambo ya kipindi cha kikafiri, Hizbiyyah na badala yake wakusanyike juu ya Tawhiyd na imani.

[1] 49:13

[2] Imaam Ahmad katika ”al-Musnad” (23489).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 62-66
  • Imechapishwa: 22/08/2018