11. Kujisalimisha na kuyakubali maandiko kuhusu sifa za Allaah

Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Kila kilichokuja katika Qur-aan au kimesihi kutoka kwa Mteuliwa (´alayhis-Salaam) kuhusiana na sifa za Mwingi wa rehema, basi ni wajibu kukiamini na kukipokea kwa kujisalimisha na kukikubali na kuacha kuyatupilia mbali, kuyapindisha maana, kuyashabihisha na kuyafananisha.

Kuhusiana na yanayotatiza katika hayo, ni wajibu kuyathibitisha kimatamshi[1] na kuacha kuyaingilia sana kwa undani maana. Sambamba na hilo tunamrudishia ujuzi wake kwa Aliyeyatamka na kujaalia jukumu lake kwa yule aliyelisimulia – hilo ni kwa kufuata njia ya wale wenye msingi madhubuti katika elimu ambao Allaah kawasifu katika Kitabu Chake cha wazi pale aliposema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا

“Na wale wenye msingi madhubuti katika elimu husema: “Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Mola wetu.””[2]

Upande mwingine Amewaraddi wale wanaotaka kupotosha na kuharibu Uteremsho Wake wa Aayah zisizokuwa wazi:

فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

”Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotevu hufuata zile zisizokuwa wazi ili kutafuta fitina na kutafuta kuzipotosha – na hakuna ajuae uhakika Wake isipokuwa Allaah.”[3]

Amefanya kutafuta kuzipotosha ni alama ya upotevu na akaliambatanisha hilo na kukusudia kutafuta fitina. Halafu vilevile akawafungia kwa yale waliyoyatarajia na akaponda ndoto zao kwa yale waliyoyakusudia pale aliposema (Subhaanah):

وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ

”Na hakuna ajuae uhakika Wake isipokuwa Allaah.”

MAELEZO

Mgawanyiko wa maandiko yanayozungumzia sifa za Allaah na sampuli za watu juu yake

Maandiko ya Qur-aan na Sunnah yanayozungumzia sifa za Allaah yamegawanyika aina mbili:

1 – Yaliyo wazi kabisa.

2 – Yasiyokuwa wazi na yamefichika.

Yaliyo wazi ni yale ambayo matamshi na maana yake iko wazi. Katika hali hiyo ni lazima kuyaamini kimatamshi na kuthibitisha maana yake kikweli pasi na kuyarudisha nyuma, kuyapindisha maana, kuyafananisha wala kuyapigia namna. Yametajwa na Shari´ah. Kwa hiyo ni lazima kuyaamini na kuyapokea kwa kuyakubali na kujisalimisha.

Kuhusu yanayotatiza ni yale ambayo maana yake haiko wazi kutokana na ujumla wa majulisho yake au upungufu wa uelewa wa mwenye kuyasoma. Ni lazima kuthibitisha tamko lake kwa sababu limetajwa na Shari´ah, kukomeka inapokuja katika maana yake na kuacha kuyaingilia sana kwa undani maana. Kwa sababu ni yenye kutatiza. Hatuwezi kutoa hukumu juu yake. Hivyo tunarudisha ujuzi wake kwa Allaah.

[1] Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aalish-Shaykh (Rahimahu Allaah) amesema kuhusiana na maneno ya mtunzi ”ni wajibu kuyathibitisha kimatamshi”:

“Hili ambalo limesemwa na mtunzi, ni katika mambo ambayo kakosolewa katika kitabu hichi. Kuna maneno mengi ambayo mtunzi wa kitabu amekosolewa. Kwa sababu inatambulika ya kwamba madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuamini yaliyothibiti katika Kitabu na Sunnah kuhusiana na majina na sifa za Allaah kimatamshi na kimaana. Mtu anatakiwa kuamini kuwa majina na sifa hizi ni za ukweli na sio kwa njia ya mafumbo (Majaaz) na kwamba hizo zote zina maana ya hakika na kweli inayolingana na utukufu na ukubwa wa Allaah. Dalili ya hayo ni nyingi kiasi cha kwamba haziwezi kudhibitiwa. Maana ya majina haya ni kwa udhahiri wake na yanatambulika kutoka katika Qur-aan kama yalivyo mengine. Hakuna kinachotatiza wala kubabaisha. Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamechukua kutoka kwake Qur-aan na wakanakili kutoka kwake Hadiyth. Hawakutatizwa na kitu katika maana ya Aayah na Hadiyth hizi kwa sababu ziko wazi na dhahiri. Vivyo hivyo wale waliokuja baada yao katika zile karne bora. Kama ilivyopokelewa kutoka kwa Maalik wakati alipoulizwa kuhusu maneno Yake (Subhaanah):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

Akasema:

”Kulingana kunatambulika, namna haijulikani, ni lazima kuamini hilo na ni Bid´ah kuuliza juu yake.”

Vivyo hivyo inapokelewa maana kama hiyo kutoka kwa Rabiy´ah ambaye ni mwalimu wake Maalik na yanapokelewa kutoka kwa Umm Salamah ambaye amesimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hali ya kutoka kwa Swahabah.

Ama uhakika wa sifa yenyewe na namna yake, hakuna anayejua hilo isipokuwa Allaah (Subhaanah) pekee. Kwa sababu kuzungumzia sifa ni sehemu katika kumzungumzia yule Mwenye kusifiwa nazo. Kama ambavo hakuna anayejua namna alivyo isipokuwa Yeye pekee basi vivyo hivyo sifa Zake. Hii ndio maana ya maneno yake Maalik:

“Namna haijulikani.”

Kuhusu maneno aliyoyataja katika ”al-Lum´ah” yanaendana na madhehebu ya Mufawwidhwah. Ndio madhehebu maovu na machafu zaidi. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ni imamu katika Sunnah. Ni mtu aliyejitenga mbali zaidi na madhehebu ya Mufawwidhwah na wazushi wengine. Allaah ndiye mjuzi zaidi.” (Fataawa wa Rasaa´il Samaahat-ish-Shaykh Muhammad bin Ibraahiym”, (1/202-203))

Yule atakayerudi katika tungo za mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) basi atajua kwa uhakika kabisa ya kwamba amejitenga mbali kabisa na madhehebu ya Mufawwidhwah na Ahl-ut-Ta´wiyl na khaswa kitabu chake ”Dhamm-ut-Ta´wiyl” ambacho amewaraddi Ahl-ut-Ta´wiyl na wale waliofuata mkondo wao katika Mufawwidhwah na ndani yake amethibitisha madhehebu ya Ahl-us-Sunnah ambayo ni kuamini yale majina na sifa zilizothibiti ndani ya Qur-aan na Sunnah kimatamshi na kimaana.

Yale yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn Qudaamah hapa aliposema:

”Ni wajibu kuyathibitisha kimatamshi.”

ni maneno yaliyokuja kijumla na yasiyokuwa wazi ambayo yamefasiriwa waziwazi na kwa ubainifu katika tungo zake zengine. Kwa hivyo ni lazima kurudi katika maneno yake (Rahimahu Allaah) yaliyo wazi. Kila kilichopokelewa kutoka kwake ambacho kinaweza kuwa na maana nyingi basi kinatakiwa kurudishwa katika maneno yake yaliyo wazi katika tungo zake nyingine. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[2] 03:07

[3] 03:07

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 31-33
  • Imechapishwa: 11/10/2022