Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Himdi zote zinamstahikia Allaah Mwenye kusifiwa na kila ulimi na Mwenye kuabudiwa katika kila zama. Ambaye elimu Yake imeenea kila mahali na wala Hashughulishwi na kitendo kutokana na kitendo kingine. Ametakasika kuwa na vyenye kumshabihi, washirika, wake na watoto. Hukumu Yake inawazunguka waja wote. Akili na mawazo hayawezi kumtambua kwa kumfikiria na wala nyoyo haziwezi kumdhibiti kwa kumuelezea:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

”Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Ana majina mazuri na sifa kuu:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَمَا تَحْتَ الثَّرَىٰ إِن تَجْهَرْ بِالْقَوْلِ فَإِنَّهُ يَعْلَمُ السِّرَّ وَأَخْفَى

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi. Ni Vyake pekee vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini na vilivyomo baina yake na vile vilivyomo chini ya udongo. Na ukinena kwa jahara; basi [tambua kuwa] Yeye anajua ya siri na yanayofichika zaidi.”[2]

Elimu Yake imekizunguka kila kitu. Vilevile ana ufalme juu ya viumbe wote kwa hukumu, huruma na elimu Yake imekienea kila kitu:

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا

“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na hawawezi kumzunguka kwa kumtambua.”[3]

Anasifiwa kwa yale Aliyojisifia Mwenyewe katika Kitabu Chake Kitukufu na kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtukufu.

MAELEZO

Lum´ah husemwa kwa kuachiwa na kukakusudiwa maana nyingi. Miongoni mwa maana hizo ni tosha ya maisha. Maana hii ndio inayonasibiana zaidi na maudhui ya Kitabu hiki. Maana ya Lum´at-ul-I´tiqaad hapa tosha ya I´tiqaad sahihi inayoendana na madhehebu ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum).

I´tiqaad ni hukumu ya kiakili ya kukata. Ikiafikiana na vile ilivyo sawa ndio sahihi. Vinginevyo itakuwa mbovu.

Yale yaliyokusanywa na mahuburi ya kitabu. Mahubiri ya mtunzi wa kitabu yamekusanya yafuatayo:

1 – Kuanza kwa Basmalah kwa ajili ya kuigiliza Qur-aan na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maana ya ´kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu` ni kwamba naanza kitu hali ya kutaka msaada na kutafuta baraka kwa kila jina katika majina ya Allaah (Ta´ala) anayesifika kwa rehema iliyokunjufu. Maana ya ´Allaah` ni Mwenye kuabudiwa hali ya kupendwa, kutukuzwa, kufanywa mola na kwa shauku. ar-Rahmaan ni Mwenye rehema kunjufu. ar-Rahiym ni anayemfikishia rehema Zake amtakaye katika viumbe Wake. Tofaouti kati ya Mwingi rehema na Mwenye kurehemu ni kwamba hiyo ya kwanza ni kwa kuzingatia kwamba rehema ni wasifu Wake na hiyo ya pili ni kwa kuzingatia kwamba ni kitendo Chake anachomfikishia amtakaye katika viumbe Wake.

2 – Kumsifu Allaah kwa himdi. Himdi ni kule kutaja sifa kamilifu za yule msifiwa na matendo Yake yenye kusifiwa pamoja na kumpenda na kumtukuza.

3 – Allaah ni Mwenye kusifiwa kwa kila ndimi na ni Mwenye kuabudiwa katika kila zama. Kwa msemo mwingine ni Mwenye kustahiki na anayefaa kuhimidiwa kwa kila lugha na kuabudiwa kila maeneo.

4 – Kuenea kwa ujuzi wa Allaah kwa sababu hakuna mahali inakosekana utambuzi Wake na ukamilifu wa uwezo Wake na kuyazunguka Kwake mambo kwa vile hatatiziki kwa jambo kutokamana na jambo jingine.

5 – Utukufu, kiburi Chake na kuwa juu Kwake kutokana na kila kinachofanana Naye na mwenza kutokana na ukamilifu wa sifa Zake kwa njia zote.

6 – Unamtakasa kutokamana na kila mke na mtoto kutokana na ukamilifu wa utajiri Wake.

7 – Ukamilifu wa kutaka Kwake na ufalme Wake kwa kupitisha hukumu Yake kwa viumbe Wote. Haimzuii nguvu za mfalme, wingi wa idadi wala mali.

8 –  Utukufu wa Allaah zaidi ya anavyofikiriwa kwa njia ya kwamba akili haiwezi kumlinganisha wala nyoyo haziwezi kumfikiria sura Yake. Kwa sababu Allaah:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

”Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[4]

9 – Allaah ana majina mazuri na sifa kuu ambazo ni maalum Kwake.

10 – Kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi. Nako ni kule kuwa Kwake juu yake na kuthibiti Kwake juu yake kwa njia inayolingana Naye.

11 – Kuenea kwa ufalme Wake wa mbingu na ardhini, vilivyo kati yao na vilivyomo chini ya ardhi.

12 – Kuenea kwa utambuzi Wake, nguvu za utawala Wake na hukumu Yake na kwamba viumbe hawawezi kumzunguka kiujuzi kutokana na upungufu wa ufahamu wao juu ya yale majina na utukufu anaostahiki Mola Mtukufu.

[1] 42:11

[2] 20:05-07

[3] 20:110

[4] 42:11

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 27-31
  • Imechapishwa: 11/10/2022