11. Hakuchinjwi kwa ajili ya Allaah mahali ambapo kunachinjwa kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

لاَ تَقُمْ فِيهِ أَبَدًا

“Usisimame huko kamwe!” (at-Tawbah 09:108)

2- Thaabit bin adh-Dhwahhaak (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna mtu aliweka nadhiri ya kuchinja mahali kunapoitwa Bawaanah. Akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu hilo ambapo akasema: “Je, mahali hapo kulikuwepo sanamu lolote katika masanamu ya kipindi cha kikafiri likiabudiwa?” Wakasema: “Hapana.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, kulikuwepo sikukuu yoyote iliyofanywa katika sikukuu zao?” Wakasema: “Hapana.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Tekeleza nadhiri yako. Kwani hakika hakuna kutekeleza nadhiri katika kumuasi Allaah wala katika kitu ambacho hakimiliki mwanaadamu.”[1]

Ameipokea Abu Daawuud na cheni ya wapokezi wake iko kwa mujibu wa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.

MAELEZO

Anachomaanisha na mlango huu ni kwamba haijuzu kwa waumini kujifananisha na watenda maasi wala kuwepo sehemu za maasi na sehemu za ´ibaadah za makafiri hata kama itahusiana na mambo mengine mbali na kuchinja. Haya ili mtu asinasibishwe nao na akashirikishwa nao. Mtu akichinja mahali ambapo kunachinjwa kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah basi anaweza kunasibishwa na watu waovu au akadhiniwa vibaya. Muumini anatakiwa kujiepusha na yote hayo.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

لاَ تَقُمْ فِيهِ أَبَدًا

“Usisimame huko kamwe!”

Aayah hii iliteremshwa kuhusiana na msikiti wa Dhwiraar uliojengwa na wanafiki kwa ajili ya kuwalinda baadhi ya makafiri. Walikuwa wakikusanyika huko na wakisaidizana juu ya namna gani watamuua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hata hivyo wakayaficha hayo. Badala yake wakadhihirisha kuwa wameujenga msikiti kwa ajili ya kuwasaidia madhaifu na masikini wakati wa nyusiku za wakati wa majira ya baridi. Wakamuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aswali ndani yake kabla ya kwenda Tabuuk. Lakini akawataka udhuru na kuwaambia kwamba ataswali ndani yake pale ataporudi kutoka Tabuuk. Wakati alipokuwa njiani anarudi nyumbani ndipo Allaah akamteremshia yenye kufedhehesha na kubainisha njama zao mbaya. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawatuma watu kwenda kuubomoa.

Hiyo ina maana kwamba sehemu ambazo kunafanywa kufuru na upotevu zinatakiwa kuondoshwa na kutobakizwa ili zisisaidie kueneza ufisadi. Mtunzi wa kitabu ametumia kama dalili kuonyesha kwamba sehemu ambazo kunachinjwa au kuswaliwa kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah au kunafanywa maasi zinatakiwa zisibakizwe ili zisije kuwaharibu waislamu na kunasibishwa nao. Hiki ni kipimo, Qiyaash, kilichothibiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Huenda mtoto wako huu asili yake ni hivo.”[2]

 2- Thaabit bin adh-Dhwahhaak (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna mtu aliweka nadhiri ya kuchinja mahali kunapoitwa Bawaanah. Akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu hilo ambapo akasema: “Je, mahali hapo kulikuwepo sanamu lolote katika masanamu ya kipindi cha kikafiri likiabudiwa?” Wakasema: “Hapana.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, kulikuwepo sikukuu yoyote iliyofanywa katika sikukuu zao?” Wakasema: “Hapana.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Tekeleza nadhiri yako. Kwani hakika hakuna kutekeleza nadhiri katika kumuasi Allaah wala katika kitu ambacho hakimiliki mwanaadamu.”[3]

Bawaanah ni sehemu ilioko kusini mwa Makkah. Imesemekana vilevile kwaba iko karibu na Yanbuu´.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “Je, mahali hapo kulikuwepo sanamu lolote katika masanamu ya kipindi cha kikafiri likiabudiwa?” na “Je, kulikuwepo sikukuu yoyote iliyofanywa katika sikukuu zao?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichelea asije kuwa amefanya sehemu hiyo kuwa maalum kwa sababu kuna mzimu katika mizimu ya kipindi cha kikafiri au sikukuu miongoni mwa sikukuu zao na kwamba muulizaji anataka kuwaiga. Wakati alipojuzwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba hakuna mambo hayo ndipo akamwamrisha kutekeleza nadhiri yake. Ni dalili inayofahamisha kwamba ni wajibu kutekeleza nadhiri ikiwa mtu lengo lake sio kujifananisha na washirikina, makafiri na mfano wao.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “Kwani hakika hakuna kutekeleza nadhiri katika kumuasi Allaah”. Kwa mfano mtu akaweka nadhiri ya kunywa pombe. Haifai kuitekeleza. Wanachuoni wametofautiana kama ni wajibu kuitolea kafara ya kiapo. Maoni ya kwanza yanasema kuwa ni nadhiri batili na kwamba haina kafara. Dalili zao ni zile zenye kuenea. Lakini hata hivyo kumekuja mapokezi mengi yanayofahamisha juu ya uwajibu wa kuitekeleza. Haya ndio maoni ya pili na ndio yenye nguvu.

Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “wala katika kitu ambacho hakimiliki mwanaadamu”. Kwa mfano mtu akaweka nadhiri kwa jina la Allaah kumwacha mtumwa wa fulani. Nadhiri hii ni batili.

Kwa kifupi ni kwamba haitakikani kwa muumini kufanya ´ibaadah sehemu za kipindi cha kikafiri au sehemu za shirki na maasi isipokuwa kukibadilishwa na kukafanywa kwa mfano msikiti au kukajengwa nyumba au kukaondoshwa athari za kipindi cha kikafiri. Katika hali hiyo itakuwa inafaa. Kama ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyoamrisha avunjwe al-Laat na badala yake kujengwe msikiti sehemu hiyo[4]. Katika hali hiyo itafaa kufanya ´ibaadah mahali hapo.

Kukifanywa shirki au Bid´ah makaburini haina maana kwamba haitofaa kuyatembelea makaburi hayo kwa mujibu wa Shari´ah. Kama ambavo haitokatazwa kuswali kwenye msikiti ambapo kunafanywa maasi.

´Umar bin al-Khattwaab aliamrisha kuswali makanisani kwa sababu manaswara ni wenye kuyafanya ni sehemu ya kumuabudia Allaah. Lakini ´ibaadah zao zina makosa na hazina maana yoyote na ndani yake zina shirki. Huenda alisema hivo kwa sababu ni wenye kuyafanya ni sehemu ya kumuabudia Allaah, au kwa sababu waislamu walikuwa ni wenye kulazimika kuswali ndani yake wakati wanaposafiri, au kwa sababu aina ya ´ibaadah ni yenye kufanana baina yao inapokuja katika swalah.

[1] Abu Daawuud (3313). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (2834).

[2] al-Bukhaariy (5305) na Muslim (1500).

[3] Abu Daawuud (3313). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (2834).

[4] Abu Daawuud (450) na Ibn Maajah (743).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 01/10/2018