10. Kuchinja kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

”Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika; na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni muislamu wa kwanza.” (al-An´aam 06:162-163)

2-

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali kwa ajili ya Mola wako na [pia ukichinja] na chinja [kwa ajili Yake]!” (at-Takaathuur 108:02)

3- ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amenieleza kuhusu mambo mane; Allaah amemlaani yule mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah. Allaah amemlaani yule mwenye kuwalaani wazazi wake wawili. Allaah amemlaani yule mwenye kumpa himaya mzushi. Allaah amemlaani yule mwenye kubadili alama ya ardhi.”

Ameipokea Muslim.

4- Twaariq bin Shihaab amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna mtu aliyeingia Motoni kwa sababu ya nzi na kuna mtu mwengine aliingia Peponi kwa sababu ya nzi.” Wakasema: “Ilikuweje, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Watu wawili waliwapitia watu waliokuwa na sanamu ambalo ilikuwa haijuzu kwa mtu yeyote kulipita mpaka mtu alitolee swadaqah. Wale watu wakamwambia mmoja wao: “Litolee swadaqah.” Akasema: “Sina chochote cha kutoa.” Wakamwambia: “Litolee ijapokuwa ni nzi.” Hivyo akalitolea nzi. Wakamwacha kwenda zake na akaingia Motoni. Wakamwambia yule mwengine: “Litolee.” Akasema: “Siwezi kamwe kutoa swadaqah kwa ajili ya yeyote yule asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall).” Hivyo wakamkata shingo yake na akaingia Peponi.”[1]

Ameipokea Ahmad.

MAELEZO

Bi maana ukhatari wa kitendo hichi na kwamba ni katika shirki kubwa, kama zilivyofahamisha dalili.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

”Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika; na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni muislamu wa kwanza.” (al-An´aam 06:162-163)

قُلْ

“Sema!”

Bi maana sema, ee Muhammad.

نُسُكِي

“… kichinjwa changu… ”

Kichinjwa. Imesemekana vilevile kwamba ni ´ibaadah zote kukiwemo kuchinja.

وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي

“… na uhai wangu na kufa kwangu… “

Bi maana zile ´ibaadah na matendo ninayoishi ndani yake ni kwa ajili ya Allaah pekee. Aayah inabainisha kwamba kuchinja ni ´ibaadah na hivyo ni lazima afanyiwe Allaah pekee na haitakikani kumfanyia mwingine. Yule mwenye kumchinjia mwingine asiyekuwa Allaah kama vile jini, masanamu na wafu waliyomo ndani ya makaburi ni kama mfano wa mwenye kuswali kwa ajili ya asiyekuwa Allaah. Kwa sababu swalah na kuchinja yote mawili ni ´ibaadah kwa kwa vile Allaah ameyataja kwa pamoja na kusema:

وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ

“… na kwa hayo ndio nimeamrishwa… “

Allaah ndiye kamwamrisha.

2-

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali kwa ajili ya Mola wako na [pia ukichinja] na chinja [kwa ajili Yake]!” (at-Takaathuur 108:02)

Bi maana swali na uchinje kwa ajili Allaah kushukuru kwa ajili ya mto mkubwa Kawthar. Hii ni dalili inayofahamisha kwamba kuchinja na swalah vyote viwili ni ´ibaadah kwa sababu ameviamrisha vyote viwili. Mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah ni shirki kama ambavyo mtu ataswali kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah. Mwenye kuchinja kwa ajili ya masanamu, majini au vyenginevyo ameshirikisha.

3- ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amenieleza kuhusu mambo mane; Allaah amemlaani yule mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah. Allaah amemlaani yule mwenye kuwalaani wazazi wake wawili. Allaah amemlaani yule mwenye kumpa himaya mzushi. Allaah amemlaani yule mwenye kubadili alama ya ardhi.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameanza na: “Allaah amemlaani yule mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah” kwa sababu shirki ndio dhambi kubwa. Laana maana yake ni kuwekwa mbali na rehema za Allaah. Ni dalili inayofahamisha kwamba shirki ndio dhambi kubwa kabisa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dhambi kubwa ni kumshirikisha Allaah.”[3]

Kuwalaani wazazi wawili ni katika dhambi kubwa pia. Inahusiana vilevile na yule mwenye kuwatukana wazazi wa mtu mwingine na mtu huyo akawatukana wazazi wake. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Miongoni mwa dhambi kubwa ni mtu kuwatukana wazazi wake.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Vipi mtu atawatukana wazazi wake?” Akajibu: “Ndio. Mtu atamtukana baba wa mwingine na yeye mtu huyo amtukanie baba yake, na mtu atamtukana mama wa mwingine na yeye mtu huyo amtukanie mama yake.”[4]

Kuwatukana watu pasi na haki ni katika madhambi makubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumuua ni ukafiri.”[5]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Thaabit bin adh-Dhwahhaak maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kumlaani muumini ni kama kumuua.”[6]

Muslim amepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu wenye [kupenda] kulaani hawatokuwa mashahidi wala waombezi siku ya Qiyaamah.”[7]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “mwenye kumpa himaya mzushi”. Bi maana yule mwenye kuwalinda Ahl-ul-Bid´ah na watenda maasi na akawanusuru. Huyu amelaaniwa. Vilevile yule mwenye kuzuia wasisimamishiwe adhabu ya Kishari´ah. Kadhalika yule mwenye kusimamisha Bid´ah ba kuzinusuru.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “mwenye kubadili alama ya ardhi”. Alama hizi zinawekwa kwa ajili ya kupambanua ardhi za watu. Yule mwenye kubadili alama hizi amelaaniwa kwa sababu jambo hili linaweza kupelekea katika matatizo, mabalaa na vita. Katika hayo kunaingia vilevile zile alama zinazowaelekeza watu barabara. Yule mwenye kuzibadili amelaaniwa.

4- Twaariq bin Shihaab amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna mtu aliyeingia Motoni kwa sababu ya nzi na kuna mtu mwengine aliingia Peponi kwa sababu ya nzi.” Wakasema: “Ilikuweje, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Watu wawili waliwapitia watu waliokuwa na sanamu ambalo ilikuwa haijuzu kwa mtu yeyote kulipita mpaka mtu alitolee swadaqah. Wale watu wakamwambia mmoja wao: “Litolee swadaqah.” Akasema: “Sina chochote cha kutoa.” Wakamwambia: “Litolee ijapokuwa ni nzi.” Hivyo akalitolea nzi. Wakamwacha kwenda zake na akaingia Motoni. Wakamwambia yule mwengine: “Litolee.” Akasema: “Siwezi kamwe kutoa swadaqah kwa ajili ya yeyote yule asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall).” Hivyo wakamkata shingo yake na akaingia Peponi.”[8]

Ameipokea Ahmad.

Twaariq huyu alikuwa ni miongoni mwa Maswahabah wadogo. Mara nyingi anapokea kutoka kwa Abu Muusa al-Ash´ariy. Upokezi huu ni kupitia kwa Swahabah ambaye hakutajwa. Wakati Swahabah anapopokea kutoka kwa Swahabah mwenzie pasi na kumtaja upokezi unakuwa Swahiyh.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “kwa nzi”, bi maana kwa sababu ya nzi.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “sanamu”. Sanamu ni kitu kilichochongwa kwa sura. Kitu kilichochongwa pasi na sura huitwa “mzimu”. Masanamu pia huitwa “mizimu”.

Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “haijuzu kwa mtu yeyote kulipita”. Bi maana hawamwachi akapita.

Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kwamba mmoja wao akasema “Sina chochote cha kutoa”. Hakukemea kitendo hicho. Ndipo wakawa na matumaini kwake na wakamwamrisha alitolee swadaqah ijapo nzi tu. Kwa sababu hiyo akaingia Motoni. Hii ni dalili inayofahamisha kwamba kulitolea swadaqah sanamu hata kama itakuwa ni kitu kisichokuwa na maana yoyote ni shirki. Kwa sababu kuchinja na ´ibaadah nyenginezo hafanyiwi mwingine asiyekuwa Allaah pekee.

Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kwamba walipomuomba yule mwingine kufanya hivo akasema “Siwezi kamwe kutoa swadaqah kwa ajili ya yeyote yule asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall)”. Mtu huyu amepinga na akawabainishia kuwa kitendo hicho hakijuzu. Matokeo yake akaingia Peponi. Hili linaweza kuwa na maana mbili:

1- Katika Shari´ah yao mtu alikuwa hapewi udhuru kwa kutenzwa nguvu. Kwa ajili hiyo ndio maana hakuchukua ruhusa ili aweze kujinasua na shari yao.

2- Inawezekana vilevile aliacha kuchukua ruhusa hiyo kwa sababu ya imani na yakini yake yenye nguvu, ndipo wakamuua.

Ama katika Shari´ah yetu mtu akitenzwa nguvu kufanya shirki na akafanya kwa ajili ya kujinasua na shari yao na wakati huohuo moyo wake ukawa umetua juu ya imani yake hakuna neno. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake – isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya imani – lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao wana ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu.” (an-Nahl 16:106)

Katika hali hiyo inafaa kuchukua ruhusa hata kama atahitajia kutamka kufuru kwa ulimi wake.

 Hadiyth ya Twaariq ameipokea Ahmad katika “az-Zuhd”. Ibn-ul-Qayyim ameitaja kwa cheni ya wapokezi yenye nguvu.

[1] Ibn Abiy Shaybah (33037) kutoka kwa Salmaan, al-Bayhaqiy katika ”Shu´b-ul-Iymaan” (7343) na Ahmad katika ”az-Zuhd” (1715).

[2] Muslim (1978).

[3] al-Bukhaariy (2654) na Muslim (87).

[4] al-Bukhaariy (5973) na Muslim (90).

[5] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

[6] al-Bukhaariy (6105) na Muslim (110).

[7] Muslim (2598).

[8] Ibn Abiy Shaybah (33037) kutoka kwa Salmaan, al-Bayhaqiy katika ”Shu´b-ul-Iymaan” (7343) na Ahmad katika ”az-Zuhd” (1715).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 46-48
  • Imechapishwa: 01/10/2018