09. Kufanya Tabarruk kwa mti, jiwe na mfano wake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ أَلَكُمُ الذَّكَرُ وَلَهُ الْأُنثَىٰ

”Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat, mwengine wa tatu [mliokuwa mkiwaabudu]? Je, nyinyi mna wana wa kiume Naye ana wana wa kike?” (an-Najm 53:19-21)

2- Abu Waaqid al-Laythiy amesema:

“Tulitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuelekea Hunayn na sisi ndio bado karibuni tulikuwa tumetoka katika ukafiri. Washirikina walikuwa na mkunazi wakikaa hapo kwa muda mrefu na wakitundika silaha zao juu ambao ulikuwa ukiitwa Dhaat an-Waatw. Tukapita kwenye mti mwengine wa mkunazi tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tufanyie na sisi Dhaat an-Waatw kama ambavyo wao wako na Dhaat an-Waatw?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Allaahu ni mkubwa! Ndio zilezile njia [za makafiri]. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, kwa hakika mmesema kama walivosema wana wa israaiyl kumwambia Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ

“Tufanyie mungu kama ambavyo wao wako na miungu!” Akasema: “Hakika nyinyi ni watu wajinga!” (al-A´raaf 07:138)

Hakika mtafuata njia za wale waliokuwa kabla yenu.”[1]

Ameipokea at-Tirmidhiy na ameisahihisha.

MAELEZO

Mfano wake kunamaanisha makaburi, masanamu na vyenginevyo.

Tabarruk maana yake ni kule mtu kutafuta baraka kutoka katika vitu hivyo. Kama wanavofanya waabudu makaburi, waabudu mawe na waabudu miti. Ameacha kutaja hukumu yake ili mwanafunzi aweze kuzingatia hukumu kupitia maandiko. Hukumu ya kitendo hicho ni shirki, kama atavyotaja mwandishi. Tabarruk hii ni miongoni mwa matendo ya watu wa kipindi cha kikafiri na ni jambo linachengua Uislamu. Baadhi waliitikia, nao ni wachache, ilihali wengi walipinga:

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

“Wengi wa watu hawatoamini ijapokuwa utalitilia hima.” (Yuusuf 12:103)

Kuhusiana na kisiwa cha kiarabu wengi wao waliingia katika Uislamu baada ya kufunguliwa mji wa Makkah.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ أَلَكُمُ الذَّكَرُ وَلَهُ الْأُنثَىٰ

”Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat, mwengine wa tatu [mliokuwa mkiwaabudu]? Je, nyinyi mna wana wa kiume Naye ana wana wa kike?”

Je, masanamu haya yamenufaisha na kudhuru? Maana yake ni kwamba hayakunufaisha wala hayakudhuru. Walikuwa wakiyaabudu, wakiyaomba baraka na msaada. Matendo yanachengua Uislamu. al-´Uzzaa lilikuwa ni salamua la watu wa Makkah na majirani wao. Manaat lilikuwa ni sanamu la watu wa al-Madiynah. al-Laat lilikuwa ni sanamu la watu wa at-Twaa-if na wale wenye kuwafuata. Masanamu haya yaliondoshwa na kuvunjwa siku ileile ulipofunguliwa mji wa Makkah. Pamoja na hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hayatoenda masiku na michana mpaka aabudiwe al-Laat na al-´Uzzaa.”

2- Abu Waaqid al-Laythiy amesema:

“Tulitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuelekea Hunayn na sisi ndio bado karibuni tulikuwa tumetoka katika ukafiri. Washirikina walikuwa na mkunazi wakikaa hapo kwa muda mrefu na wakitundika silaha zao juu ambao ulikuwa ukiitwa Dhaat an-Waatw. Tukapita kwenye mti mwengine wa mkunazi tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tufanyie na sisi Dhaat an-Waatw kama ambavyo wao wako na Dhaat an-Waatw?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Allaahu ni mkubwa! Ndio zilezile njia [za makafiri]. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, kwa hakika mmesema kama walivosema wana wa israaiyl kumwambia Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ

“Tufanyie mungu kama ambavyo wao wako na miungu!” Akasema: “Hakika nyinyi ni watu wajinga!” (al-A´raaf 07:138)

Hakika mtafuata njia za wale waliokuwa kabla yenu.”[2]

Ameipokea at-Tirmidhiy na ameisahihisha.

Maneno yake “na sisi ndio bado karibuni tulikuwa tumetoka katika ukafiri” hii ni aina fulani ya udhuru. Ni kama vile anataka kusema kwamba ndio maana hatukujua kitendo hichi.

Maneno yake “wakitundika silaha zao juu” kwa ajili ya kutafuta baraka. Wanadai kwamba wakifanya hivo basi silaha zinakuwa na nguvu na makali sana.

Maneno yake “Tufanyie na sisi Dhaat an-Waatw kama ambavyo wao wako na Dhaat an-Waatw” bi maana ili nao waweze kupata baraka.

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakasirika na kusema: “Allaahu ni mkubwa!” Hii ilikuwa ni ada yake pindi anapoona jambo analolilekea basi husema: “Allaahu ni mkubwa!” au “Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu”. Hii ndio Sunnah pindi mtu anapoona jambo analolikemea au jambo lililompendeza. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema: “Nyinyi ni robo ya watu wa Peponi” Maswahabah wakasema: “Allaahu ni mkubwa!”[3]

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ndio zilezile njia [za makafiri]” bi maana za kuabudu miti, mawe na kufanya Tabarruk kwa vitu hivyo. Huu ndio mfumo unaotambulika kwa watu waliotangulia hapo kale. Kwa msemo mwingine ndio mfumo wa watu tangu hapo kale na siku zote walikuwa ni wenye kufanya hivo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “mmesema kama walivosema wana wa israaiyl”. Israaiyl, Israel, ni Ya´quub mwana wa Ishaaq mwana wa Ibraahiym.  Wana wa israaiyl ni mayahudi ambao wanajinasibisha na israaiyl, israel. Mayahudi walimwambia Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ

“Tufanyie mungu kama ambavyo wao wako na miungu!” Akasema: “Hakika nyinyi ni watu wajinga!”

Muusa akawakaripia na akawakumbusha Tawhiyd. Vivyo hivyo Maswahabah hawa waliwaiga wale kwa sababu ya ujinga. Hawakuwa wanajua hukumu ya kitendo hichi kwa sababu punde tu ndio wametoka katika ukafiri. Hii ni dalili inayofahamisha kwamba kinachozingatiwa ni uhalisia wa mambo na sio matamshi. Kwa sababu wameomba kitu ili wakiadhimishe na watafute baraka kwacho kama walivofanya wana wa israaiyl japokuwa matamshi yao ni yenye kutofautiana. Batili ni batili ijapokuwa matamshi ni yenye kutofautiana.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Hakika mtafuata njia za wale waliokuwa kabla yenu.” Bi maana mienendo yao. Hii ina maana kwamba Ummah huu utapewa majaribio kama walivyopewa majaribio watu walioshi katika kipindi cha kikafiri katika kuiabudu miti na mawe na kufanya Tabarruk kwavyo. Haya tayari ni mambo yamekwishatokea. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema hivo ili kueleza kwamba yatatokea. Ametahadharisha mambo hayo na akaashiria kwamba jambo la wajibu ni kuwa na thabati katika kumuabudu Allaah peke yake kama walivyofanya Mitume. Ama kuyaabudu makaburi ni miongoni mwa matendo ya mayahudi, manaswara na washirikina wengine.

[1] Ahmad (21947), at-Tirmidhiy (2180), Ibn Hibbaan (6702) na at-Twabaraaniy (3291). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (5408).

[2] Ahmad (21947), at-Tirmidhiy (2180), Ibn Hibbaan (6702) na at-Twabaraaniy (3291). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (5408).

[3] al-Bukhaariy (3348) na Muslim (222).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 43-45
  • Imechapishwa: 01/10/2018