Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Imesihi kupokelewa kutoka kwa Abu Bashiyr al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba alisafiri mara kadhaa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akaagiza mjumbe kupeleka ujumbe usemao:

“Pasiachwe katika shingo ya ngamia kidani cha kamba au mkufu isipokuwa kikatwe.”[1]

2- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika matabano, hirizi na Tiwalah ni shirki.”[2]

Ameipokea Ahmad na Abu Daawuud.

3- ´Abdullaah bin ´Ukaym amepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayevaa/atakayejifungamanisha na kitu basi huwakilishwa kwacho.”[3]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy.

Hirizi ni kitu huvalishwa watoto ili kimkinge na kupatwa na kijicho. Lakini ikiwa kilichotundikwa ni kitu kilicho na Qur-aan, basi wako baadhi ya Salaf ambao wameonelea kuwa inaruhusu na baadhi yao wengine, akiwemo Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) pia, wameona kuwa hairuhusu na wamefanya kuwa ni katika mambo yaliyokatazwa.

Matabano ndio ile inayoitwa “formula”. Kuna dalili zinazofahamisha kwamba matabano yasiyokuwa na shirki yanafaa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameruhusu kujitibu kwa matabano dhidi ya kijicho na homa.

Tiwalah ni kitu kinachotengenezwa na wanadai kwamba humpendezea mke kwa mume wake au mume kwa mke wake.

4- Ahmad amepokea kutoka kwa Ruwayfiy´ ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinambia: “Ee Ruwayfiy´! Huenda ukaishi muda mrefu. Hivyo waeleze watu kwamba ambaye anazifunga fundo ndevu zake, akatundika kidani cha kamba ya upinde au akajisafisha kwa choo cha mnyama au mfupa, basi hakika Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko mbali naye.”[4]

5- Sa´iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kukata hirizi kutoka kwa mtu atakuwa ni kama ambaye kaacha mtumwa huru.”[5]

Ameipokea Wakiy´.

6- Amepokea vilevile kwamba Ibraahiym amesema:

“Walikuwa wakichukizwa na hirizi zote; ni mamoja za Qur-aan na zisizokuwa za Qur-aan.”[6]

MAELEZO

1- Mlango unaozungumzia maandiko yaliyokuja kuharamisha hirizi na kupambanua kuhusu matabano. Kuna baadhi ambao wameharamisha hirizi za aina fulani na wamehalalisha za aina nyingine. Maoni sahihi ni kwamba hirizi zote ni haramu. Hirizi ni kitu kinachoninginizwa kwa mtoto dhidi ya kijicho. Dalili zimefahamisha kwamba ni haramu, kama itavyokuja huko mbele kwa mgonjwa na mtoto.

2- Kuhusu matabano, kunahitajia maelezo. Inafaa kwa kupatikana sharti tatu:

1- Iwe kwa lugha yenye kufahamika kwa Aayah za Qur-aan na du´aa zenye kutambulika.

2- Isiwe na kitu kinachopingana na Shari´ah.

3- Asiamini kwamba yenyewe ndio inayonufaisha. Katika Hadiyth iliyotangulia imekuja:

“Matabano yanafaa midhali ndani yake hamna shirki.”

Tiwalah mwandishi ameeleza maana yake. Ni jambo linalofanywa kwa kuchukua msaada kutoka kwa majini na mashaytwaan. Wanaita “uchawi”, “uvutwaji”, “ukimbizaji”. Uchawi wote ni ukafir:

إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru.” (al-Baqarah 02:102)

3- ´Abdullaah bin ´Ukaym amepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayevaa/atakayejifungamanisha na kitu basi huwakilishwa kwacho.”

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy.

Mtu anatakiwa kumtegemea Allaah pekee. Hili ndilo jambo litalomnufaisha pamoja vilevile na kufanya sababu. Kama ilivyokuja katika Hadiyth:

“Pupie kile kinachokunufaisha na taka msaada kwa Allaah (´Azza wa Jall) na wala usikate tamaa.”[7]

Kufanya sababu ni jambo la lazima katika kuomba du´aa, kufuata Shari´ah ya Allaah, kutafuta sababu zitazomfanya mtu kupona na kutafuta riziki. Kufanya sababu ima ikawa ni wajibu au jambo lenye kujuzu. Kwa hiyo mtu anatakiwa kuhakikisha amefanya zile sababu zenye kujuzu na za wajibu. Kufanya hivo hakuitii kasoro Tawhiyd ya mtu. Bali mambo ni kinyume chake.  Kuacha kufanya sababu kunatia kasoro akili na Tawhiyd vyote viwili.

Hirizi ikiwa ni ya Qur-aan wako baadhi ya Salaf waliojuzisha hilo, kama ´Abdullaah bin ´Amr, wengine wakaikataza, kama ´Abdullaah bin Mas´uud. Maoni haya ya mwisho ndio ya sawa yanayofahamishwa na dalili. Lililo la wajibu ni kufunga mlango huu kwa ajili ya kuzuia njia zote zinazopelekea katika shirki na kutendea kazi dalili. Haitakiwi kuwavalisha watoto hirizi. Bali mtu anatakiwa awasomee du´aa kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivomsomea al-Hasan na al-Husayn[8].

Wako baadhi ya Salaf ambao wameandika Qur-aan katika karatasi na kwenye sahani. Imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbas, lakini haikuthibiti. Hata hivyo haina neno. Ibn-ul-Qayyim ametaja katika “Zaad-ul-Ma´aad”. Hata hivyo matabano ndio bora zaidi.

Kujitibisha pia hakuna neno. Imekuja katika Hadiyth:

“Enyi waja wa Allaah! Jitibisheni na wala msijitibishe kwa kitu cha haramu.”[9]

Maoni sahihi ni kwamba imependekezwa. Maalik amesema:

“Ni jambo liko sawasawa.”

Bi maanal limeruhusiwa.

4- Ahmad amepokea kutoka kwa Ruwayfiy´ ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinambia: “Ee Ruwayfiy´! Huenda ukaishi muda mrefu. Hivyo waeleze watu kwamba ambaye anazifunga fundo ndevu zake, akatundika kidani cha kamba ya upinde au akajisafisha kwa choo cha mnyama au mfupa, basi hakika Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko mbali naye.”

Hapa kuna mambo mane:

1- “…ambaye anazifunga fundo ndevu zake… “ Wanachuoni wamesema kuwa maana yake ni kwamba mtu anazifunga ndevu zake kwa kuzitengeneza kwa ajili ya  kutafuta kiburi na ukuu. Imesemekana vilevile kwamba ili mtu asijifananishe na wanawake na mashoga. Kuhusu kuzijali kwa kuzichanua na kuzihudumia hakuna neno. Katika Hadiyth kuna udhaifu lakini hata hivyo imepokelewa kupitia zengine zinazoitolea ushahidi.

2-  “… akatundika kidani… “ Kinachotengenezwa kwa matumbo na vyengine. Wakati wa kabla ya kuja Uislamu walikuwa wakiwaninginiza ngamia na watoto ili wasipatwe na kijicho.

3- “… au akajisafisha kwa choo cha mnyama au mfupa… “. Kuna Hadiyth zimekuja zikikataza mambo hayo. Kwa sababu ni mambo yasiyosafisha na isitoshe ni kujifananisha na kipindi kabla ya kuja Uislamu.

4- “… basi hakika Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko mbali naye…. “ Hapa kuna makemeo makali. Hata hivyo haina maana kwamba anakuwa mshirikina. Hadiyth hii ni kama mfano wa Hadiyth isemayo:

“Si katika sisi yule anayejipiga kwenye mashavu, kuchana nguo zake au akaita kwa wito wa kipindi kabla ya kuja Uislamu.”

Kinacholengwa hapa ni kukatazwa kutundika kidani, uzi na vyengine ambavo mtu anadhani kuwa vinanufaisha. Lililo la wajibu ni mtu kumtegemea Allaah pekee.

5- Sa´iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kukata hirizi kutoka kwa mtu atakuwa ni kama ambaye kaacha mtumwa huru.”

Ameipokea Wakiy´.

Wakiy´ bin al-Jarraah alifariki 196.

Katika Hadiyth kuna fadhilah za kukata hirizi na kwamba ni sawa na kuacha mtumwa huru. Kwa sababu katika hali hii amemsalimisha mtumwa huyu kutokamana na Moto na shirki. Kwa ajili hiyo inakuwa ni bora kuliko kuacha mtumwa huru kwa kujitolea mwenyewe. Inawezekana maneno haya ya Sa´iyd yamepokelewa kupitia cheni ya wapokezi. Ni jambo ambalo lina wasaa ndani yake kwa sababu Sa´iyd hazungumzi hivo kutoka kichwani mwake. Inawezekana vilevile kwamba alitamka hivo kutokana na Ijtihaad na uelewa wake. Lakini baada ya uhakiki na upekuzi imeonyesha kwamba kitendo hicho ni bora zaidi kuliko kumwacha mtumwa huru kwa kujitolea mwenyewe.

Kutundika hirizi ni shirki ndogo na ni jambo lenye khatari kubwa. Inaweza vilevile kupelekea katika shirki kubwa.

6- Amepokea vilevile kwamba Ibraahiym amesema:

“Walikuwa wakichukizwa na hirizi zote; ni mamoja za Qur-aan na zisizokuwa za Qur-aan.”

Anaitwa Ibraahiym bin Yaziyd an-Nakha´iy. Ni mtu aliyekuja baada ya Maswahabah (Taabi´iy) na alikuwa ni mwanafunzi wa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Walikuwa wakichukizwa na hirizi na vivyo hivyo mwalimu wao Ibn Mas´uud. Alikuwa anachukizwa na jambo hilo kutokana na sababu mbili:

1- Hadiyth zimekuja kwa njia ya jumla.

2- Kwa sababu kufunga njia zote zinazopelekea katika shirki. Kwa hivyo haitakiwi kutundika Qur-aan, Aayah za Qur-aan, Hadiyth, talasimu wala mifupa. Yote haya ni shirki.

[1] al-Bukhaariy (3005) na Muslim (2115).

[2] Abu Daawuud (3883), Ibn Maajah (3530), Ahmad (3615), at-Twabaraaniy (10503) na al-Bayhaqiy (19387). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (331).

[3] at-Tirmidhiy (2027), an-Nasaa’iy (4079) na Ahmad (18803). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaamiy´” (12477).

[4] Abu Daawuud (36), an-Nasaa’iy (5067) na Ahmad (17037). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (13869).

[5] Ibn Abiy Shaybah (23473).

[6] Ibn Abiy Shaybah (23467).

[7] Muslim (2664).

[8] al-Bukhaariy (3371).

[9] Abu Daawuud (3874), at-Twabaraaniy (649) na al-Bayhaqiy (19465). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (2643).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 39-42
  • Imechapishwa: 01/10/2018