12. Kuweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah ni katika shirki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ

“Ambao wanatimiza nadhiri zao.” (al-Insaan 76:07)

2-

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ

”Na chochote mtoacho katika matumizi au mkiwekacho nadhiri katika nadhiri, basi Allaah anakijua.” (al-Baqarah 02:270)

3- Imepokelewa Swahiyh kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuweka nadhiri ya kumtii Allaah na amtii na mwenye kuweka nadhiri ya kumuasi Allaah na asimuasi.”[1]

MAELEZO

Bi maana ni katika shirki kubwa. Hii ni shirki iliokuwa ikifanywa katika kipindi cha kikafiri na inafanywa na waabudu makaburi ambao wanayawekea nadhiri makaburi na kuyataka uokozi na mengineyo. Mitume wametumilizwa ili kukataza shirki hii iliouwa ikifanywa katika kipindi cha kikafiri. Ama shirki ndogo ni kama mfano wa kujionyesha, kuapa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema “akitaka Allaah  na wewe”.

1-

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ

“Ambao wanatimiza nadhiri zao.”

Hapa wanasifiwa wale waumini ambao wanazitekeleza nadhiri zao nzuri zilizoafikiana na Shari´ah. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa nadhiri ni ´ibaadah ambayo ni wajibu kumtekelezea nayo Allaah pekee.

2-

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ

”Na chochote mtoacho katika matumizi au mkiwekacho nadhiri katika nadhiri, basi Allaah anakijua.”

Ina maana kwamba Allaah anajua matumizi na nadhiri za waja. Allaah anawalipa kwayo ikiwa yamefanywa kwa ajili Yake. Ni dalili inayofahamisha kuwa nadhiri ni ´ibaadah kwa sababu imetajwa pamoja na matumizi. Matumizi, kama kuwapa swadaqah mafukara na masikini, ni ´ibaadah yakitolewa kwa ajili ya Allaah. Mtu akiliwekea nadhiri au kulitolea swadaqah kaburi, kujengwa kwake au waungu maalum, kitendo hicho kinakuwa ni shirki kubwa.

3- Imepokelewa Swahiyh kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuweka nadhiri ya kumtii Allaah na amtii na mwenye kuweka nadhiri ya kumuasi Allaah na asimuasi.”

Hii ni dalili inayofahamisha kwamba ni wajibu kutekeleza nadhiri ambayo ni ´ibaadah kwa Allaah. Mfano wa hilo ni kama mtu kusema:

“Najifaradhishia mwenyewe kufanya kitu kadhaa kwa ajili ya Allaah.”

Kuhusiana na nadhiri ya maasi haifai kuitekeleza.

[1] al-Bukhaariy (6696).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 51
  • Imechapishwa: 01/10/2018