Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Hatumkufurishi yeyote katika waislamu kwa sababu ya dhambi na wala hatumtoi katika Uislamu kwa sababu ya kitendo chake.

Tunaonelea kuwa hajj na Jihaad vitaendelea kuwepo na viongozi wote, ni mamoja kiongozi huyo awe ni mwema au muovu. Vilevile inajuzu kuswali swalah ya ijumaa nyuma yao. Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo matatu ni katika msingi wa imani: Kukomeka na aliyetamka “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” hatumkufurishi kwa dhambi wala kumtoa katika Uislamu kwa kitendo na Jihaad itaendelea kuwepo tangu aliponituma Allaah (´Azza wa Jall) mpaka pale Ummah wangu wa mwisho utapompiga vita ad-Dajjaal – hayaangushwi na unyanyasaji wa mwenye kunyanyasa wala uadilifu wa mwenye kufanya uadilifu. Aidha kuamini Qadar.”[1]

Imepokelewa na Abu Daawuud.

MAELEZO

Ahl-ul-Qiblah ni waislamu wanaoswali kuelekea Qiblah. Hawakufurishwi kwa kutenda madhambi makubwa na wala hawatolewi nje ya Uislamu kwa sababu hiyo na wala hawadumishwi milele ndani ya Moto. Amesema (Ta´ala):

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا

“Ikiwa makundi mawili ya waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini moja wapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni kati yao.”[2]

mpaka alipofikia kusema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ

“Hakika si vyenginevyo waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni baina ya ndugu zenu.”[3]

Amethibitisha udugu wa kiimani licha ya kupigana ambayo ni dhambi kubwa. Ingelikuwa ni ukafiri basi kungekanushwa udugu wa kiimani.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

 “Yule ambaye moyoni mwake mlikuwa na imani sawa na mbegu ya hardali mwondosheni.”

Bi maana Motoni.

Kuna maafikiano juu yake.

[1] Abu Daawuud (2532), al-Bayhaqiy (9/159) na wengine. Katika cheni ya wapokezi yupo Yaziyd bin Abiy Nashbah na hajulikani, hilo limetajwa katika ”at-Taqriyb”. Tazama al-Mundhiyr “Mukhtaswar Sunan Abiy Daawuud” (3/380).

[2] 49:09

[3] 49:10

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 148-149
  • Imechapishwa: 15/12/2022