Katika Aayah hii kuna mazingatio na hukumu kubwa. Ni wajibu kwa muislamu aizingatie na kuitafakari ili asitumbukie katika kitu kilichotahadharishwa. Mambo haya yanafanywa na watu wengi hii leo. Dini, wanachuoni, Sunnah na Qur-aan kuchezewa shere. Leo haya yanafanywa kwa wingi. Wako wanaosema kwamba Qur-aan na Sunnah ni mambo hayaendani na watu katika wakati huu na kwamba Sunnah haitumiwi kama hoja na kwamba eti ni mapokezi yamepokelewa na watu, kama wanavosema, na kwamba haitumiwi kama hoja. Wana maneno mengine kama hayo yanayotia aibu.

Hali kadhali yanayoandikwa kwenye magazeti na yanarushwa katika vyombo vya mawasiliano katika kuiponda dini ya Uislamu na kuishambulia. Mambo yanayofanywa leo ni mengi. Yangelikuwa haya yanafanywa na makafiri jambo hili lingekuwa sahali. Kwani hakuna dhambi nyingine kubwa baada ya kufuru. Lakini kwa masikitiko makubwa haya yanafanywa na baadhi ya wale ambao wanajinasibisha na Uislamu  na wanadai kuwa na elimu. Wanaponda hukumu za Kishari´ah, Aayah au dalili za Kishari´ah na wanasema eti zinaweka shaka na wala hazifidishi kitu isipokuwa dhana tupu na kwamba eti hazifidishi elimu na mfano wa maneno kama haya ya kufuru. Wengine wanawasema vibaya wanachuoni na kwamba eti ni wanachuoni wa hedhi na nifasi, wanachuoni wa wafalme na kwamba ni wapakanaji mafuta. Wana maneno mengne machafu wanayoyarudirudi na kuyaandika yasiyofichikana. Yote haya yanaingia katika Aayah hii tukufu. Yule mwenye kufanya hivo juu yake kuna matishio aliyoyataja Allaah katika Aayah hii. Allaah amesema kuwa makafiri wanawafanyia maskhara na kuwaponda waumini. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ  وَإِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمُ انقَلَبُوا فَكِهِينَوَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ

”Hakika wale waliofanya ukhalifu walikuwa [duniani] wakiwacheka wale walioamini. Na wanapowapitia [karibu yao], basi wanakonyezana. Na wanaporudi kwa ahli zao, hurudi [huku wakiwa] wenye kushangilia. Na wanapowaona, basi husema: “Hakika hawa ndio waliopotea bila shaka.” (al-Mutwaffifiyn 83:29-32)

Wanasema kuwa waumini eti wamepotea na kwamba dini kama hii ni ya upotevu, imekudanganyeni na kwamba ni makosa na sio ya sawa kwa kuwa haiendani na wakati na maendeleo na kwamba eti iko nyuma.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 134-135
  • Imechapishwa: 24/12/2018