103. Uwajibu wa kukemea na kutokaa mahali yanaposemwa vibaya mambo kuhusu dini

La nane: Miongoni mwa mambo ya ajabu ni kwamba aliyeongea ni mtu mmoja katika majlisi. Lakini hata hivyo Allaah akafanya hukumu ni yenye kuwaenea wote. Amesema:

أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” (at-Tawbah 09:65-66)

Amejaalia kuwa wote wamefanya istihzai. Kwa nini? Kwa sababu wale wengine waliokuwa pale hawakukataza na ndipo hukumu ikawakusanya wote. Wakinyamazia maovu nao wanashiriki pamoja na aliyefanya uovu huo. Kwa ajili hii pindi kijana huyu alipokataza alitakasika na dhambi hii na Allaah akateremsha Aayah katika Qur-aan kumuunga mkono. Ama wale wengine hawakukaripia. Hii ni dalili inayofahamisha kwamba yule anayehudhuria majlisi za kufuru, dini inachezewa shere, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah na wanachuoni na wala hakemei hukumu ni yenye kumgusa pia. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

”Unapowaona wale wanaoziingilia na kuzishambulia Aayah Zetu, basi jitenge nao mpaka waingie kwenye mazungumzo mengineyo. Na kama shaytwaan akikusahaulisha, basi baada ya kukumbuka usikae pamoja na watu madhalimu.” (al-An´aam 06:68)

وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّـهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ إِنَّكُمْ إِذًا مِّثْلُهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا

”Naye amekwishakuteremshieni katika Kitabu kwamba mnaposikia Aayah za Allaah zinakanushwa na zinafanyiwa istihzai, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengineyo. Vinginevyo mtakuwa kama wao. Hakika Allaah atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika Moto wa Jahannam.” (an-Nisaa´ 04:140)

Ni dalili ioneshayo ya kwamba yule ambaye hakatazi mahali ambapo anatukanywa Allaah, Mtume, Maswahabah, wanachuoni au dini anakuwa kama yule mwenye kutukana. Wote wanapata hukumu moja. Kwa sababu Allaah amejaalia kufanya istihzai  ni kwa wote pamoja na kwamba mwongeaji ni mmoja tu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 133-134
  • Imechapishwa: 24/12/2018