Malaika wako sampuli mbalimbali. Wako ambao kazi yao ni kulinda matendo ya wanadamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Pale wanapopokea wapokeaji wawili wanaokaa kuliani na kushotoni. Hatamki maneno yoyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha [kurekodi].”[1]

Wanaandika matendo ya mwanadamu ya kheri na ya shari. Wanafanya hivo kwa amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hawa ndio watukufu wenye kuandika waliotajwa katika maneno Yake (Ta´ala):

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ كِرَامًا كَاتِبِينَ يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ

“Hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi; watukufu wanaoandika. Wanajua yale myafanyayo.”[2]

Huandika matendo ya wanadamu na hupishana usiku na mchana. Kuna Malaika ambao wanakuwa na mwanadamu kipindi cha mchana, wengine wanakuwa naye kipindi cha usiku. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanapishana kwenu Malaika wa usiku na Malaika wa mchana. Wanakusanyika katika swalah ya Fajr na swalah ya ´Aswr. Halafu hupanda wale waliolala kwenu ambapo Mola wenu Anawauliza – ilihali ni mjuzi zaidi kuliko wao: “Mmewaachaje waja Wangu?” Wanasema: “Tumewaacha na huku wanaswali na tumewaendea na huku wanaswali.”[3]

Mambo yanakuwa namna hii siku zote. Kwa ajili hii kisomo cha Fajr kinatakiwa kiwe kirefu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا

“Simamisha swalah jua linapopinduka hadi kiza cha usiku na Qur-aan ya alfajiri. Hakika Qur-aan ya alfajiri ni yenye kushuhudiwa.”[4]

Ndio maana swalah ya Fajr ikaitwa kuwa ni “kisomo” kwa sababu hurefushwa ndani yake kisomo. Qur-aan ya Fajr ni yenye kushuhudiwa maana yake ni kwamba inahudhuriwa na Malaika wa usiku na Malaika wa mchana. ´Aswr ndio swalah ya kati na kati na ndio swalah bora kabisa. Nayo pia inahudhuriwa na Malaika wa usiku na Malaika wa mchana. Allaah (Ta´ala) amesema:

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ

“Zichungeni swalah na khaswa swalah ya katikati na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu.[5]

[1] 50:17-18

[2] 82:10-12

[3] al-Bukhaariy (7429).

[4] 17:78

[5] 2:238

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 78-80
  • Imechapishwa: 31/08/2021