1 – Kutoa ni mapenzi na jambo lenye kusifiwa kama ambavo ubakhili ni chukivu na jambo lenye kusimangwa. Hakuna kheri katika mali isipokuwa kwa kuitoa.

2 – Ukarimu bora ni kule mtu kujitolea mali yake na akajiepusha na mali za wengine. Anayejitolea anakuwa bwana. Anayefanya ubakhili anakuwa mbaya.

3 – Ubakhili ni mti wa Motoni ambao matawi yake yako duniani. Yule mwenye kushikilia tawi miongoni mwa matawi yake basi yatamvuta kumwelekeza Motoni. Ukarimu ni mti wa Peponi ambao matawi yake yako duniani. Yule mwenye kushikilia tawi miongoni mwa matawi yake basi yatamvuta kumwelekeza Peponi. Pepo ni makazi ya wakarimu.

4 – Hakuna sifa inayomdhalilisha na kumtweza mtu na dini yake kama ubakhili.

5 – Naafiy´ amesema:

“Wakati Ibn ´Umar alipoumwa al-Madiynah alitamani zabibu wakati ambao hazikuwa zikipatikana. Wakaenda kuzitafuta na hawakuzipata isipokuwa kwa bwana mmoja. Akanunua zabibu nyingi kwa dirhamu moja. Akaja mwombaji na akaamrisha azipewe pasi na yeye kuzionja.”

6 – Sijamuona yeyote mashariki na magharibi ambaye ni mkarimu na si mwenye kuwaudhi watu isipokuwa alianza kuwaongoza watu wote. Yule anayetaka ngazi ya juu Aakhirah na ngazi ya juu duniani basi alazimiane na kutoa na aache kuwaudhi watu. Na yule anayetaka kudhalilisha na kukiuka utu na dini yake, kuwachosha ndugu zake na kuwakera majirani zake basi alazimiane na ubakhili.

7 – Ubakhili ulisimangwa na watu wenye busara katika kipindi cha kikafiri na katika Uislamu mpaka hii leo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 235-242
  • Imechapishwa: 31/08/2021