Watumiaji hawa wa akili wanasema kuwa yale mambo yanayokushindeni kuyafasiri, ijapo kwa njia ya mbali na ya kigeni, basi chukueni msimamo wa kuyanyamazia. Lakini itakidini kuwa kilichokusudiwa sio ule udhahiri wake na kwamba Allaah pekee ndiye anayejua maana yake. Hii ndio ´Aqiydah ya Mufawwidhwah. Maana yake ni kuwa Allaah ametuteremshia mafumbo na kitendawili ambacho hatukijui. Allaah ameteremsha Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu, hakuiteremsha ili iwe kama mafumbo na kitendawili. Ni kweli kwamba maana ya baadhi ya maandiko yanaweza kutofahamika kwa baadhi ya watu, lakini watu hawa wanatakiwa kurejea kwa wanazuoni na watu wenye utambuzi. Watu ambao ni wajuzi zaidi juu ya Qur-aan na Sunnah baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Maswahabah, wanafunzi wao na vile vizazi bora. Kwa hivyo inatakiwa kurejea katika maneno na tafsiri zao. Hii ndio njia ya sawa, njia ya haki:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema… ”

Bi maana wamewafuata katika maneno, vitendo na tabia zao.

رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ

”… Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye.”[1]

Wamezipata radhi za Allaah – na hili ndio lengo!

[1] 9:100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 148-149
  • Imechapishwa: 03/09/2024