104. Hawataki turejee katika Qur-aan na Sunnah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Nimeona wengi katika wao wakiweka wazi maana ya maneno haya. Yanapelekea katika mambo yasiyoepukika na maana yake ni kwamba Qur-aan haimwongozi mtu katika kumtambua Allaah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatakiwi kufundisha na kuelezea juu ya sifa za Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba watu wakati wa kukhitilafiana hawatakiwi kuyarudisha waliyokhitilafiana kwa Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), bali warudi katika mfano wa yale waliyokuwemo katika kipindi cha kishirikina kabla ya kuja Uislamu, katika mfano wa yale ambayo wanahukumiana kwayo ambao hawawaamini Mitume, kama mfano wa wabrahmini na wanafalsafa (ambao ni washirikina), waabudia moto na baadhi ya wasabai. Hata hivyo kurejea kwao si jengine isipokuwa kuifanya hali kuwa mbaya zaidi na hakuondoi tofauti yoyote.

MAELEZO

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) anasema kwamba wako waliosema waziwazi kuwa Qur-aan haifahamishi katika haki yoyote. Mmoja katika mabwanyenye wao[1] amefikia kusema kuwa ”Kitaab-ut-Tawhiyd” cha Ibn Khuzaymah kimekuja na shirki na si Tawhiyd. Kwa nini anaona kuwa Ibn Khuzaymah amefikisha shirki? Kwa sababu Ibn Khuzaymah anathibitisha majina na sifa za Allaah, ambazo zinapatikana kati ya viumbe. Kwa hivyo wanaona eti kuzithibitisha ni shirki. Wanasema eti kumthibitishia Allaah majina na sifa kunapelekea kuwa wanashirikiana na Allaah katika umilele na kutokuwa na mwisho. Kwa msemo mwingine wanaona kuwa wa milele hatokuwa Allaah pekee. Wanaona kuwa hiyo ni shirki. Na wale miongoni mwao ambao hawakusema wazi yaliyoko hapo juu hawana njia ya kuyakwepa isipokuwa kuafikiana nayo, kwa sababu hawakufanya kurejea katika Qur-aan na Sunnah.

Ijapo Radd hii ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika kitabu hiki haiwazidishii kitu isipokuwa tu ukaidi na kung´ang´ania maoni yao. Kwa sababu wao malengo yao sio kuitafuta haki. Wao kazi yao ni kujadili kwa batili ili kuitokomeza haki, ingawa Allaah (Azza wa Jall) ameifanya Qur-aan ni yenye kuondosha makinzano. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[2]

Upande wa pili wao wanaona kuwa Qur-aan na Sunnah haviondoshi tofauti.

[1] Naye si mwengine ni al-Fakhr ar-Raaziy wakati wa kufasiri kwake 42:11. Tazama ”at-Tafsiyr al-Kabiyr” (27/130).

[2] 4:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 149-150
  • Imechapishwa: 03/09/2024