Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Wanaona kuwa ndio haki na yale yote yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah yanayoenda kinyume na mawazo yao si jengine isipokuwa tu ni mtihani kutoka kwa Allaah. Makusudio sio eti nyinyi myaamini lakini ni kwa ajili mjitahidi wenyewe kwa kutumia vipengele vya lugha, matamshi matupu na maneno ya kigeni. Kunyamaza, hali ya kuegemeza ujuzi wake kwa Allaah na sambamba na hilo kukanusha kuwa yanafahamisha sifa yoyote ndio uhakika wa ´Aqiydah ya wanafalsafa hawa.

MAELEZO

Maneno yao yanapelekea kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameiteremsha Qur-aan ili kuzitahini akili zao juu yake – ni nani mwenye kupatia na ni nani mwenye kukosea? Ni kama kwamba Qur-aan ni mtihani peke yake na sio uongofu. Hivo ndivo yanavopelekea fikira yao. Ni nani kati yenu anayeijua haki kwa akili yake na ni nani kati yenu asiyeijua haki kwa akili yake? Kisha wanafikia kwamba mtu analazimika kuchukua msimamo wa kunyamaza na ´Aqiydah ya kutegemeza utambuzi wa maandiko kwa Allaah. Wanaifasiri Qur-aan kwa maneno ya kigeni, kwa njia za mbali na kwa lugha zilizosuswa. Mwishowe wanadai kuwa wamefikia katika yale yaliyokusudiwa na Allaah. Hii maana yake ni kuwatuhumu watu kushindwa na kuwatia katika upotofu. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Mwingi wa huruma na Mwenye kuwarehemu waja Wake. Anajua unyonge wao. Anatambua unyonge wa fahamu zao. Kwa ajili hiyo hakuwategemeza katika akili zao. Badala yake amewaamrisha kufuata Wahy. Yule anayejua elimu sahihi juu ya Wahy, basi aifanyie kazi. Yule asiyejua basi awaulize wanazuoni na asipekue jambo asilolijua.

Hii leo kuna maoni ya ajabu. Wanalingania katika uhuru wa maoni. Inasema kwamba kila mmoja aseme kile anachotaka. Ni kana kwamba hatuna Wahy na wala hatuna Shari´ah. Kana kwamba yote tu ni maoni. Maoni yangu na maoni yako. Niache na maoni yangu na mimi nikuache na maoni yako. Kila mmoja afate maoni yake. Huu ndio upotevu. Mimi, wewe na fulani na fulani tunarejea katika Kitabu cha Allaaah. Tunatakiwa kuyapima maoni yetu na Kitabu cha Allaah. Maoni yanayosapotiwa na Wahy ni sahihi, na yale maoni yanayopingana na Wahy ni batili na ni wajibu kujirejea nayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[1]

Ni bora kwenu kuliko kuingia katika vurugu. Kwa sababu Wahy Allaah (´Azza wa Jall) ameukinga na makosa, ama maoni na fikira zenu – hazikukingwa na makosa. Yanafikwa na makosa na kasoro.

[1] 4:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 147-148
  • Imechapishwa: 03/09/2024